Saudi Arabia yafanya mashambulizi ya anga Yemen
26 Machi 2015Kikosi cha anga cha Saudi Arabia Alhamisi (26.03.2015)kimedhibiti anga ya Yemen masaa machache baada ya kuanza kwa operesheni yake hiyo iliopewa jina "Kimbunga cha Moto" kwa kushambulia kambi za kijeshi zinazodhibitiwa na Wahouthi.
Mashambulizi hayo yalilenga mji mkuu wa Sanaa unaodhibitiwa na Wahouthi na kuharibu bohari za silaha na kuuwa viongozi kadhaa wa waasi hao.Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Al Arabiya mashambulizi hayo yalifanyika Jumatano usiku wa manane baada ya Wahouthi na jeshi linalowaunga mkono kuingia katika mji wa kusini wa Aden ambao ni ngome kuu ya Rais wa Yemen anayepigwa vita na waasi hao Abd Rabu Mansour Hadi.
Wanamgambo wanaomuunga mkono Hadi leo wameukombowa uwanja wa ndege wa Aden baada ya vikosi vinavyowaunga mkono Wahouthi kurudi nyuma kutoka uwanja wa ndege huo kufuatia mapigano makali.
Ushawishi wa Iran
Nchi nyingi zenye idadi kubwa ya Waislamu wa madhehebu ya Sunni zina wasi wasi kwamba kuanguka kwa utawala wa Hadi nchini Yemen kutazidi kuimarisha ushawishi wa nchi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ya Iran ambayo inaaminika kuwa inawaunga mkono Wahouthi ambao pia ni Washia.
Balozi wa Saudi Arabia nchini Marekani Adel al Jubeir amesema hatua hiyo ya kijeshi dhidi ya Wahouthi ni kuunga mkono wananchi wa Yemen na serikali yao halali.
Nchi nyengine za Kiarabu zikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu,Kuwait,Bahrain,Jordan, Morocco na Sudan zinajiunga katikia mapambano hayo dhidi ya Wahouthi ambao wameteka sehemu kubwa ya Yemen katika miezi ya hivi karibuni.
Wito wa Hadi waitikiwa
Operesheni hiyo inayozishirika zaidi ya nchi 10 inatokana na wito wa Rais Hadi kutaka msaada wa kuwadhibiti waasi wa Kihouthi.Marekani imedhinisha msaada wa vifaa na taarifa za ujasusi kwa operesheni hiyo.
Hapo jana utawala wa Hadi wa miaka mitatu ulionekana unafikia kikomo wakati Wahouthi na washirika wake walipokuwa wakiukaribia mji wa Aden.Serikali ya Yemen imekanusha repoti kwamba rais huyo ameikimbia nchi hiyo kwa kusema kwamba yuko mahala salama katika mji huo wa bandari.
Iran imetaka kusitishwa mara moja kile ilichokiita uvamizi wa kijeshi na kuonya kwamba utazidi kuupalilia mzozo huo wa Yemen.
Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/Reuters
Mhariri :Josephat Charo