1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sasa wakimbizi Syria kama wa Rwanda 1994

17 Julai 2013

Maafisa wakuu wa Umoja wa Mataifa wamearifu kuwa mgogoro wa wakimbizi unaosababishwa na vita vya Syria ndio mkubwa zaidi kutokea tangu ule wa wakati wa mauaji ya kimbari nchini ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

https://p.dw.com/p/199Qq
Mkimbizi wa Syria nchini Jordan
Mkimbizi wa Syria nchini JordanPicha: picture-alliance/dpa

Taarifa kuhusu mgogoro wa kibinadamu unaosababishwa na vita vinavyoendelea nchini Syria, zilitolewa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Jumanne. Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Antonio Guterres alisema kuwa tatizo la wakimbizi wa Syria limefikia kiwango cha kutisha.

''Kwa sasa wapo wakimbizi wa Syria wapatao milioni 1.8, waliosajiliwa na shirika letu katika eneo ilipo Syria. Theluthi mbili za wakimbizi hao waliikimbia nchi yao kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu, kwa wasitani wa wakimbizi 6000 kila siku. Hatujawahi kushuhudia mtiririko wa wakimbizi kwa kiasi hicho, tangu yalipotokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda, miaka takribani 20 iliyopita.'' Alisema Guterres.

Guterres alisema kukubaliwa kwa wakimbizi na nchi za Jordan, Iraq na Lebanon, kumesaidia kuokoa maisha ya maelfu ya watu.

Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa UNHCR
Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa UNHCRPicha: Reuters

Watu milioni 4 wahitaji msaada wa haraka

Mratibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya Dharura Valerie Amos ambaye pia alilihutubia Baraza la Usalama, alisema jumuiya ya kimataifa inatafakari uwezekano wa operesheni ya msaaada yenye kuvuka mpaka, ili kuwafikia wenye mahitaji ndani ya Syria.

Alisema watu milioni 4 ndani ya Syria wanahitaji msaada wa haraka, na kwamba mashirika ya kiutu yaliyoko huko yanakabiliwa na vikwazo vikubwa kutoka upande wa serikali, na wa waasi. Amos alisema kuwa bado dola bilioni 3.1 zinahitajika kuweza kuwahudumia wakimbizi wa Syria hadi mwishoni mwa mwaka huu.

Valerie Amos alisema hali ni mbaya zaidi katika mji wa Homs, ambao ulikumbwa na mapigano makali wakati serikali ilipoendesha operesheni za kuukomboa mwezi uliopita, akisema anaamini raia 2,500 wamenaswa ndani ya mji huo.

Valerie Amos, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada wa Dharura
Valerie Amos, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada wa DharuraPicha: Ebrahim Hamid/AFP/Getty Images

Wapatao 5000 hufariki kila mwezi

Vita hivyo ambavyo sasa vimedumu kwa muda wa miaka 2, vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 100,000, hiyo ikiwa kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamu Ivan Simonovic, amesema kuwa watu wapatao 5000 hupoteza maisha nchini Syria kila mwezi kutokana na vita hivyo, na kuonya kuwa hiyo ni ishara ya kwamba mgogoro unazidi kuwa mbaya.

Balozi wa Syria kwenye Umoja wa Mataifa Bashar Jaafar amepinga ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya vifo nchini mwake, akisema imetokana na vyanzo visivyoaminika, akisema haikuwa sahihi kulipa kandarasi shirika la kimarekani kukusanya takwimu hizo.

Mgogoro huo sasa umevuka mpaka na kuungana na ule wa kimadhehebu unaoendelea katika nchi jirani ya Iraq, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa mwakilishi wa Umoja wa Mataifa mjini Baghdad, Martin Kobler. Kobler alisema kuwa wa-Iraq sasa wanapigana wenyewe kwa wenyewe ndani ya makundi ya waasi nchini Syria, na kuonya kuwa iwapo hakuna hatua za haraka zitakazochukuliwa, hali hiyo itafika kiwango ambacho hakiwezi kudhibitiwa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/AP
Mhariri: Ssessanga, Iddi Ismail