Sasa ni hakika NATO kujitoa Afghanistan 2014
22 Mei 2012Wasi wasi uliokuwapo ni kwamba rais wa sasa wa Ufaransa Francois Hollande angeyaondoa na mapema majeshi ya nchi yake kutoka Afghanistan. Lakini baada ya mkutano wa NATO wasi wasi huo umeondoka na kwamba Ufaransa itaendelea kutoa ushirikiano.
Mpango wa kujitoa wathibitishwa
Viongozi wa NATO jana waliweka utaratibu wa kujitoa kutoka katika vita ambavyo haviungwi mkono na watu wengi nchini Afghanistan, wakiunga mkono mipango ya kukabidhi uongozi wa mapambano kwa Waafghan wenyewe kuanzia katikati ya mwaka 2013 huku wakitilia mkazo kuwasaidia wakati nchi hiyo ikielekea katika kuchukua udhibiti wa kila kitu.
Katika azimio lililotolewa katika mkutano wa Chicago , rais wa Marekani Barack Obama pamoja na washirika wake wa kijeshi wa NATO waliidhinisha mpango maalum ambao hautabadilika wa kujitoa taratibu lakini kwa utaratibu maalum wa uwajibikaji kwa kuondoa wanajeshi 130,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2014.
Waafghanistan hawatakuwa peke yao
Rais Obama ameuambia mkutano huo kuwa wakati Waafghanistan wanasimama kuchukua jukumu la nchi yao hawatakuwa peke yao.
"Wakati Waafghanistan wanasimama, hawatasimama peke yao. Leo tumekubaliana juu ya uhusiano wa muda mrefu wa NATO na Afghanistan kupindukia mwaka 2014, ikiwa ni pamoja na msaada wetu kwa majeshi ya usalama ya Afghanistan."
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesisitiza kuwa haoni hatari yoyote, kuhusiana na msimamo wa Ufaransa kwamba huenda kutakuwa na hali ya mataifa mengine kujitoa kutoka Afghanistan iwapo Ufaransa ingejitoa. Kwa hiyo NATO imethibitisha mpango wake kwa ajili ya Afghanistan.
Ufaransa pia itasaidia
Hata baada ya mwaka 2014 NATO itaendelea kuwapo nchini Afghanistan, kwa kazi ya elimu, ushauri na usaidizi. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesema:
"Hii ina maana ya misingi sahihi ya kisheria kupitia azimio la umoja wa mataifa, kwa ujumbe huu unaoongozwa na NATO, ujumbe ambao hautakuwa wa mapambano, ambao utakuwa na wajibu wa kutoa ushauri na usaidizi, wakati huo huo ukiwa na wajibu pia wa kutoa msaada wa elimu ambapo ni uwekezaji wa muda mrefu."
Hata hivyo muda wa kubakia nchini humo utapaswa kuidhinishwa tena na bunge la Ujerumani mwakani 2013.
Mwandishi : Bergmann, Christina / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman