Sarkozy na Merkel wakubaliana kuhusu msaada wa Ugiriki
18 Juni 2011Mpango huo unahusisha sekta binafsi kuchangia mfuko wa kuziokoa nchi zisifilisike kwa njia ya mikopo ya hiari.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amekuwa akishinikiza wawekezaji binafsi kuchangia hadi theluthi moja ya msaada huo mpya, lakini alikubali kuafikiana na Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy. Thamani ya sarafu ya Euro ilipanda kufuatia mkutano huo mjini Berlin.
Inatathminiwa kuwa Ugiriki inahitaji msaada wa Euro bilioni 80 hadi 120 ili kuepuka kufilisika, baada ya msaada wa mwaka uliopita na hatua kali za mageuzi kushindwa kurejesha imani ya masoko.
Mkutano wa viongozi hao wawili mjini Berlin utafuatiwa na mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika wiki ijayo mjini Brussels.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE,AFP)
Mhariri: Prema Martin