Sarkozy ahukumiwa kifungo cha miaka mitatu
17 Mei 2023Matangazo
Mahakama hiyo imesema anastahili kutumikia kifungo cha nyumbani cha mwaka mmoja akiwa amevalia bangili ya kielektroniki.
Sarkozy aidha amepigwa marufuku kushikilia wadhifa wowote wa umma kwa kipindi cha miaka mitatu kufuatia kitendo chake cha kujaribu kumshawishi jaji katika kesi iliyokuwa inamkabili, ushawishi alioufanya ukiwa uligunduliwa kwa njia ya udukuzi.
Sarkozy, mwenye umri wa miaka 68 aliondoka mahakamani akiwa kimya ila wakili wake akasema watakata rufaa dhidi ya uamuzi huo katika mahakama ya juu zaidi ya rufaa nchini Ufaransa.
Tangu kuondoka madarakani, Sarkozy ambaye alikuwa kiongozi wa nchi hiyo kati ya mwaka 2007 hadi 2012, amekuwa akiandamwa na kesi.