Saratani yaongezeka duniani
4 Februari 2014Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyozinduliwa mjini Lyon, Ufaransa, siku ya Jumatatu (tarehe 3 Februari) licha ya maendeleo makubwa katika kuwapatia wagonjwa matibabu, idadi ya vifo inahofiwa itaongezeka pia kutoka watu milioni 8.2 mwaka 2012 hadi kufikia milioni 13 mwaka 2030.
Hata hivyo, WHO inasema kwenye ripoti hiyo kwamba zaidi ya nusu ya wenye maradhi ya saratani wangeweza kukingwa, "ingekuwa maarifa yaliyopatikana hadi sasa yanatekelezwa ipasavyo."
"Nchi zenye pato la chini la wastani ndizo zitakazoathirika zaidi kwa sababu nyingi yake hazina vifaa vinavyofaa kukabiliana na wimbi la idadi ya wagonjwa wa saratani," amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Margaret Chan, alipokuwa anatangaza ripoti hiyo iliyochapishwa na Kituo cha utafiti wa Kimataifa kuhusu Saratani, ambayo ni taasisi maalum ya Shirika hilo yenye makao yake mjini Lyon.
Takwimu za kutisha
Ripoti hiyo yenye zaidi ya kurasa 600 na iliyopewa jina la "Ripoti ya Kimataifa kuhusu Saratani kwa Mwaka 2014" imeandaliwa kwa msaada wa wataalamu 250 kutoka nchi 40.
Mnamo mwaka 2012, watu wenye ya saratani ya mapafu ndio waliokuwa wengi zaidi, wakifikia milioni 1.8, sawa na asilimia 13 ya wagonjwa wote wa saratani, wakifuatiwa na wenye saratani ya maziwa, ambao walikuwa milioni 1.7 sawa na asilimia 11.9 na saratani ya utumbo mpana.
Saratani ya mapafu imedhihirika ndio chanzo cha vifo vingi kati ya wagonjwa wa saratani. Watu milioni 1.6 walifariki dunia kutokana na maradhi hayo mnamo mwaka 2012, hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 19.4 ya vifo vyote vilivyosababishwa na saratani. Inafuatiwa na saratani ya ini, ambao watu 800,000 walipoteza maisha na saratani ya utumbo iliyosababisha vifo vya watu 700,000 mnamo mwaka 2012.
Aina mpya za saratani
"Kutokana na sababu za ukuaji na kuzeeka wakaazi pamoja pia na vyanzo vyenginevyo mfano wa tumbaku, hali inaweza kuwa mbaya zaidi miongo inayokuja na hivyo kugeuka kuwa mtihani mkubwa kwa mfumo wa afya katika nchi zenye mapato ya chini na zile zenye mapato ya wastani," ameonya Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Saratani, Christopher Wild.
Mbali na saratani ambayo kawaida husababishwa na uvimbe kama vile saratani ya ini, utumbo au kifuko cha uzazi, sasa kumeongezeka saratani ya mapafu, ya ziwa na ya utumbo mpana yanayotokana na athari za kuvuta sigara, ulevi, unene, ukosefu wa mazoezi ya mwili na kutumia vyakula vya makopo - mtindo ulioenea sana katika nchi tajiri.
Zaidi ya nusu ya wagonjwa wapya milioni 14 waliobainika mwaka 2012, walipatikana katika nchi za Asia, hasa China. Barani Ulaya, robo ya wakaazi wake wanaugua saratani, Marekani kila raia mmoja katika watano ana ugonjwa huo na barani Afrika na Mashariki ya Kati ni asilimia 8 ya wakaazi wa huko.
Ili kukabiliana na changamoto ya kifedha (mnamo mwaka 2010 gharama za mwaka kukabiliana na maradhi ya saratani zilikadiriwa kufikia euro bilioni 858), ripoti hiyo ya WHO inashauri watu wasitegemee pekee aina mpya ya matibabu, lakini wabuni pia kinga kwa wingi.
Miongoni mwa hatua za kinga, ripoti hiyo inapendekeza kampeni za chanjo dhidi ya Hepatitis B, na dhidi ya maradhi mengineyo yanayosarabishwa na virusi ambavyo ndio chanzo cha saratani ya fuko la uzazi.
Ripoti inahimiza pia watu wasiwache kwenda kupima hata kama vifaa vya kupimia si vya kisasa sana katika baadhi ya nchi zinazoinukia.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman