Sarafu ya Uturuki Lira yapoteza thamani
13 Agosti 2018
Tunaanzia Uturuki ambako vikwazo vilivyotangazwa na rais wa Marekani Donald Trump dhidi ya mshirika huyo wa jumuia ya kujihami ya NATO, vinaanza kuleta madhara: Sarafu ya nchi hiyo Lira imepoteza asili mia 45 ya thamani yake. Gazeti la Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Baada ya mageuzi ya katiba upinzani wa kisiasa umepwaya nchini humo. Lakini sasa Recep Tayyip Erdogan anakabwa katika uwanja ule ule aupendao: uwanja wa kiuchumi. Sarafu ya Lira inapoteza thamani. Balaa hilo limezidi makali kutokana na mfumo wa kisiasa unaompatia rais madaraka makubwa zaidi.
Hakuna yeyote sasa mjini Ankara mwenye uwezo wa kuchunguza sera za Erdogan au kuzikosoa ikilazimika , kama vile mipango yake kwa benki kuu ambayo haikudurusiwa vya kutosha inavyodhihirisha. Erdogan anabidi abadilishe msimamo wake kuelekea Umoja wa ulaya na Ujerumani pia. Uturuki itaweza tu kutegemea misaada ikiwa itafuata kanuni. Na kama itatambua ukweli wa mambo. Na mojawapo ya ukweli huo ni kwamba "Mfalme amefilisika"
Netanyahu ashangiria tangu Trump aiinmgie madarakani
Serikali ya Marekani imewapa muda viongozi wa serikali ya mjini Ankara wafikirie upya matakwa yao. Katika uwanja wa kisiasa pia rais wa Marekani Donald Trump anatunisha misuli, kwa mfano mashariki ya kati, linaandika gazeti la "Rheinpfalz" :"Yote yaliyoamuliwa na Donald Trump hadi wakati huu yanaelemea kile ambacho waziri mkuu Benjamin Netanyahu daima amekuwa akikitaka. Mji wote wa Jerusalem anautambua tangu mwezi May mwaka huu kuwa mji mkuu wa Israel. Zaidi ya hayo Marekani inapigania wapalastina wasitambuliwe tena na Umoja wa mataifa kuwa wakimbizi na kwa namna hiyo itabatilishwa ile sheria inaayodhamini haki ya wapalastina kurejea katika maskani yao.
Anachokitaka Trump hasa ni kuiona Israel ikidhibtii milele sehemu kubwa ya ardhi ya wapalastina; kauli mbiu ikiwa :makubaliano ndio haya, Israel ina nguvu, kama unataka chukua hutaki basi."Rais wa utawala wa ndani wa Palastina, Mahmoud Abbas hatolikubali hilo. Na hata angetaka asingeweza. Kwasababu hapo atawaachia ushindi Hamas na hakuna anaelipendelea hilo pia."
Sera ya Umoja wa Ulaya kuelekea wakimbizi
Mada yetu ya mwisho inatufikisha mjini Brussels kumulia sera ya Umoja wa Ulaya kuelekea wakimbizi. Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" linaandika: "Kundi la wenye kujitolea ndani ya Umoja wa Ulaya linabidi liwajibike hivi sasa. Ujerumani, Ufaransa, Uhispania, Sweeden na mataifa mengineyo wanataka kuwajibika kwasababu za kiutu na pia kwa kuzingatia hali halisi namna ilivyo. Mapendekezo ya maana yametolewa. Kansela Angela Merkel atakapokutana na kiongozi mwenzake wa Uhispania Pedro Sanchez na viongozi wengineo ili kuifuata njia hiyo, mafanikio yanaweza kutarajiwa uchaguzi wa ulaya utakapoitishwa mwaka 2019. Na mzozo wa wakimbizi unaweza hatimae kuimarisha nguvu za Umoja wa Ulaya na hasa zile nchi zilizojitokeza na moyo wa kuwajibika.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman