1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sanogo: Sitagombea kwenye uchaguzi wa Mali

21 Machi 2013

Mwaka mmoja baada ya mapinduzi Mali, kiongozi wa mapinduzi hayo, Kapteni Amadou Sanogo Haya, bado anaiangalia Mali kwa matumaini japo kwenye mahojiano na DW, alitangaza kutoshiriki kwenye uchaguzi wa mwezi Julai.

https://p.dw.com/p/181GK
Coup leader Captain Amadou Sanogo attends a ceremony as former parliament speaker Dioncounda Traore (unseen) is sworn in as Mali's interim president in the captial Bamako, April 12, 2012. Traore took over as Mali's interim president on Thursday from the leaders of last month's coup, promising to hold elections and fight Tuareg and Islamist rebels occupying half the country. Traore, 70, a labour activist turned politician, was sworn in by Supreme Court President Nouhoum Tapily in the capital Bamako as part of a deal to restore civilian rule after army officers staged a March 22 coup in the West African state. REUTERS/Malin Palm (MALI - Tags: POLITICS MILITARY PROFILE)
Mali Hauptmann Amadou Sanogo in ParadeuniformPicha: Reuters

DW: Mwaka mmoja uliopita, wewe na kundi la wanajeshi wenzako muliipindua serikali ya Mali. Kwa nini?

Tulikuwa na fikra. Fikra yetu ilikuwa kwanza ni kuyarudisha maeneo yaliyokamatwa na adui wetu. Kisha tupeleke huko wanajeshi wenye utaalamu na waliofunzwa vyema kurudisha amani na kuwahakikishia raia wa Mali usalama wao. Na mwisho tulitaka kuipatia nchi hii damu mpya ya uongozi, kwani maeneo yote ya kiuchumi, kisheria na kitaaluma yalikuwa yamechafuliwa. Hapakuwa na kilichobakia, utawala ulikuwa umejaa wizi, udanganyifu na jamii ilikuwa inaporomoka. Hivyo, tulitaka kuwapa watu matumaini ya kusonga mbele.

Mwaka mmoja baadaye , sasa unaionaje hali?

Nadhani kwamba mwaka mmoja baadaye, mambo yanakaa sawa kwa kasi ndogo zaidi kuliko tulivyokuwa tumetarajia. Bila ya shaka huwezi kufanya kila kitu kwa mkupuo mmoja. Kwa dola ambayo ilikuwa imeharibiwa kwa miaka 20 au zaidi haiwezi kujengwa kwa mwaka mmoja. Hilo linaingia akilini. Lakini mtu anapaswa kukumbuka kwamba angalau maeneo yaliyokuwa yamekaliwa sasa yamerudishwa tena mikononi mwa nchi. Kuna mfumo wa kisiasa unaofanya kazi vizuri sasa. Na sasa wananchi wa Mali wameanza kufahamu kosa lililokuwa linafanyika. Yote haya yanaelezea ukweli kwamba sasa tuna fursa ya kuanza upya.

Una dhima gani sasa? Mara kadhaa umetakiwa kuachana na siasa. Namna gani unataka kutumia ushawishi wako kuyabadili mambo?

Zaidi ya furaha ya watu wa nchi hii, moyoni mwangu sioti kitu chengine cha ziada. Na sisi hatuamuliwi na wengine wala kwa ndoto za watu wengine. Tuna lengo la kitaifa, kama watoto wa nchi hii. Mambo yakienda sivyo, lazima ujuwe hilo na sio tujifiche nyuma ya magazeti na kikombe cha chai tukiwa wastaafu ambao hatuwezi kuukabili ukweli ulivyo. Kufanya hivyo ni kituko. Ama kuhusu ukosoaji kutoka nje na hoja zao kwamba napaswa kustaafu, nadhani kufanya hivyo kutaufanya utaratibu wa mageuzi uende kwa kasi ndogo.

Je utapigania, kwenye uchaguzi unaofanyika mwezi Julai ili kuhakikisha yale mambo uliyosema yalichochea mapinduzi ya kijeshi ya Machi 2012 yanatekelezeka?

Sitapigania kwenye uchaguzi huo. Hilo liko wazi kabisa.

Kapeti Amadou Sanogo Haya aliongoza uasi wa wanajeshi tarehe 21 Machi 2012 ambao ulipelekea mageuzi ya serikali na jeshi nchini Mali. Mwezi Aprili, kutokana na shinikizo kutoka mataifa jirani, alikabidhi madaraka kwa Spika wa wakati huo, Dioncounda Traoré.

Mahojiano na Yaya Konate
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohamed Abdulrahman