Salman amwambia Trump suala la Palestina litatuliwe kwa haki
7 Septemba 2020Mfalme Salman alisema hilo ni sehemu kuu ya kuanzia ya juhudi za pendekezo la amani la mataifa za Kiarabu.
Viongozi hao walizungumza kwa simu kufuatia makubaliano ya kihistoria yaliyosimamiwa na Marekani mwezi uliopita ambayo Umoja wa Falme za Kiarabu ulikubali kuwa taifa la tatu la Kiarabu kurejesha uhusiano wa kawaida na Israel baada ya Misri na Jordan.
Mfalme Salman alimwambia Trump anakubaliana na juhudi za Marekani za kuunga mkono amani na kwamba Saudi Arabia inataka kuona suluhisho la kudumu na la haki katika suala hili la Palestina chini ya juhudi za amani za mataifa ya Kiarabu zilizopendekezwa na taifa hilo mwaka 2002.
Chini ya pendekezo hilo, mataifa ya Kiarabu yamependekeza kwa Israel kurejesha uhusiano wa kawaida ili kuweza kufikiwa makubaliano ya kupatiwa Wapalestina taifa lao na Israel kujitoa kabisa kutoka katika ardhi za mataifa ya Kiarabu ilizoziteka katika vita vya mwaka 1967 vya mashariki ya kati.
Safari za ndege
Saudi Arabia, mahali palipozaliwa Uislamu na maeneo matakatifu, haiitambui Israel.
Hata hivyo, mwezi huu taifa hilo la Kifalme limesema litaruhusu safari za ndege kati ya Umoja wa Falme za Kiarbu na Israel, ikiwa ni pamoja na shirika hilo la ndege la Israel kutumia anga yake.
Mshauri wa ikulu ya Marekani na mkwe wa kiume wa Trump Jared Kushner alisema ana matumaini mataifa mengine ya Kiarabu yatarejesha uhusiano wa kawaida na Israel katika muda wa miezi michache.
Hakuna taifa lingine la Kiarabu lililosema hadi sasa kwamba linatafakari kufuata mfano wa Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mtoto wa kiume wa mfalme Salman, mwana mfalme mteule Mohammed bin Salman, na Kushner walijadili haja ya Wapalestina na Waisrael kurejea katika majadiliano na kufikia makubaliano ya kudumu ya amani baada ya Kushner kuzuru Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi uliopita.
Makubaliano kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Israel yalipingwa kwa kiasi kikubwa na palestina.