Merkel ahimiza mjadala wa kuheshimiana
31 Desemba 2017Katika hotuba yake , ambayo itatangazwa katika televisheni ya taifa leo Jumapili jioni, merkel hakutumia maneno mengi kabla ya kuelezea wasi wasi wake juu ya umoja katika jamii ya Wajerumani.
"Hakujawahi kuwa na tofauti ya mawazo kama hayo kwa muda mrefu." amesema. " Baadhi hata wanafikia wanazungumzia kuhusu kuvunjika kwa mshikamano wa jamii yetu."
Lakini mafanikio na uaminifu ni sehemu ya uhalisia wa Ujerumani kama hofu na wasi wasi, amesisitiza, na kuongeza: "Kwangu mimi , mambo yote hayo mawili yananihusu."
Merkel amesema kwamba Wajerumani wanahitaji "kutambuana zaidi, na nina maana kutambuana kweli - tusikilizane, tusikilize hasa, tuoneshe kuelewa."
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 63, ambaye kwa sasa anaongoza serikali ya mpito baada ya uchaguzi wa mwezi Septemba kusababisha mkwamo wa kisiasa, pia alitumia hotuba hiyo kama fursa ya kuwahakikishia Wajerumani kwamba anataka kuunda serikali imara haraka iwezekanavyo.
Serikali ya mseto
Vyama viwili vikubwa nchini Ujerumani , chama cha Christian Democratic Union CDU na kile cha Social Democratic SPD, vilipata pigo kwa kupoteza kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi wa Septemba 24. Chama cha SPD awali kilikataa kushitiki katika serikali mpya ya muungano mkuu na wahafidhina wakiongozwa na Merkel, lakini hivi sasa kinatafakari ombi la CDU.
Kansela ameieleza kuwa ni jukumu lake kuleta uthabiti wa kisiasa nchini Ujerumani. "Dunia haitatusubiri," ameonya.
Merkel pia alifananisha kati ya hali ya baadaye ya Ujerumani na ile ya Umoja wa Ulaya, akiyataka mataifa 27 wanachama kushikamana kama jamii moja.
"Hii itakuwa suala muhimu kwa miaka michache ijayo," amesema. Licha ya hali yake ya shaka shaka kisiasa nyumbani, Merkel alionesha mtazamo wa mbali katika hotuba yake ya mwaka mpya, akiweka malengo kwa ajili ya miaka 10 hadi 15 ijayo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nafasi zilizopo za kazi zinaendelea kuwapo, kutengeneza nafasi mpya za kazi, kuhimiza matumizi ya kidigitali na kuhimiza usawa.
"Mambo yatakwenda vizuri tu kwa Ujerumani wakati mafanikio yetu yatakapomsaidia kila mtu, na pale yatakapoboresha na kunufaisha maisha yetu," amesema, kabla ya kuwatakia afya njema wananchi na matumaini kwa mwaka 2018.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Isaac Gamba