Safari za ndege zaanza tena Iran baada ya kusitishwa
7 Oktoba 2024Mamlaka ya usafiri wa anga ya Iran ilieleza kupitia taarifa kwamba, baada ya kuhakikisha usalama kwa safari za ndege, vikwazo vyote vilivyowekwa vimeondolewa na kuwa mashirika ya ndege sasa yanaruhusiwa kuendelea kupanga ratiba zao za safari za ndege.
Vyombo vya habari vikimnukuu msemaji wa mamlaka ya usafiri wa anga viliripoti kuwa safari zote za ndege zilifutwa kutokana na vikwazo vya kiutendaji, japo bila ya kutoa maelezo zaidi.
Soma pia: Iran yaahidi kuishambulia tena Israel endapo itashambuliwa
Awali, msemaji wa mamlaka hiyo ya usafiri wa anga alieleza kuwa safari kutoka viwanja vyote vya ndege nchini humo zinasitishwa hadi saa kumi na mbili asubuhi leo Jumatatu.
Wakala wa usalama wa anga wa Umoja wa Ulaya umeyashauri mashirika ya ndege ya Ulaya kuepuka anga ya Iran angalau hadi Oktoba 31, wakati wakiendelea kutathmini hali ya usalama ya anga.
Iran ilisitisha safari zote za ndege siku ya Jumanne baada ya kuvurumisha makombora kuelekea Israel katika shambulio ambalo serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imeahidi kujibu.