Safari ya Palestina yaelekea ICC?
30 Novemba 2012Kutambuliwa kwa Palestina kama dola hata bila ya kukabidhiwa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa ni jambo ambalo linaweza kuifanya kupata uanachama katika mahakama ya Kimataifa ya jinai mjini The Hague,ambayo kwahakika ni chombo ambacho wanachama wake wanauwezo wa kuwasilisha ombi la kutaka madai ya uhalifu wa kivita au uhalifu wa kibinadamu katika nchi fulani yachunguzwe.
Kutokana na kupandishwa hadhi katika Umoja wa Mataifa sasa wapalestina huenda wakaanzisha harakati za kutuma maombi ya kutaka uanachama Icc pamoja na mamlaka ya kuwasilisha kesi ya uhalifu wa kivita dhidi ya serikali ya Israel na maafisa wake.Kitisho cha kile kinachoitwa vita vya kisheria tayari kimeanza kuwazuia baadhi ya raia wa Israel na viongozi wao wa kijeshi kusafiri nchi za nje kwa kuhofia kukamatwa kama wahalifu.
Anavyosema Robert Malley mkurugenzi wa mpango wa Mashariki ya Kati katika shirika la Kimataifa la kukabiliana na mizozo ICG ni kwamba imeshabainika kwamba Waisrael wanaogopa kufikishwa The Hague. Wapalestina walishapanga toka muda mrefu hata kabla ya ombi lao kuridhiwa kutumia nafasi ya kutokuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa kama mlango wa kubisha hodi ICC.
Mjumbe mmoja wakipalestina akizungumza na shirika la kukabiliana na mizozo duniani ameutaja mkakati huo kama vuguvugu la Intifada kwa njia ya kisheria na Kidemokrasia dhidi ya Israel.
Israel na vita dhidi ya Gaza
Mwezi Septemba wakati rais wa mamlaka ya ndani ya wapalestina Mahmoud Abbas alipouhutubia Umoja wa Mataifa aliituhumu moja kwa moja Israel kwa kuendesha uhalifu wa kivita. Miaka yote maafisa wa Israel wamekuwa wakisema vikosi vyake vya usalama vinazingatia sheria za kimataifa na kudai kwamba nia halisi ya tuhuma za Wapalestina ni kuitenga Israel.
Kilichoshuhudiwa mwaka jana ni kwamba aliyekuwa mwendesha mashitaka mkuu wa Icc Luis Moreno Ocampo alilizima ombi la Wapalestina la mwaka 2009 la kutaka Israel ifunguliwe mashtaka kwa hatua yake ya mwaka 2008 hadi mwaka 2009 katika vita vya Gaza dhidi ya kundi la Hamas.Ocampo alidai kwamba ombi la Palestina haliwezi kukubalika kwa kuwa ina hadhi ya mtazamaji tu ndani ya Umoja wa Mataifa.
Mlango wa ICC uko wazi
Mwezi Septemba Mwendesha mashitaka mkuu mpya Fatou Bensouda akatoa kauli kwamba Kura ya hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa inaweza kuleta mageuzi. Bensouda alisema walichokifanya ICC wameuacha wazi mlango ikiwa Wapalestina watafaulu kukivuka kizingiti na kutambuliwa kama dola na hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa basi bila shaka ombi lao litatathminiwa.
Mahakama hiyo ya mjini The Hague Uholanzi ni moja ya chombo cha Kimataifa ambako mtu anaweza kufunguliwa mashitaka ya uhalifu na nchi zote 117 zilizoidhinisha mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo zina haki ya kumfikisha mtuhumiwa yoyote wa makosa ya uhalifu wa kivita.
Marekani na Israel sio miongoni mwa wanachama hao lakini hilo halina maana kwamba litawazuia wapalestina kuwafikisha mbele ya chombo hicho pindi itasaini mkataba wa Roma unaoridhia kuwepo kwa ICC. Hati za ICC za ukamataji watuhimiwa pamoja na maamuzi yake ni mambo yanayobeba uzito mkubwa wa kisiasa hata ikiwa utekelezaji unashindwa.
Ni kutokana na kesi iliyofunguliwa na mahakama hiyo dhidi ya aliyekuwa kiongozi wa Libya kanali Moammer Gaddafi mwaka jana ndiko kulikosaidia Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa sauti moja kuwaunga mkono waasi waliompinga kiongozi huyo na hatimae kumuondoa madarakani na kumuangamiza.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef