Safari ya Champions League yaanza
15 Septemba 2014Real waliduwazwa mwishoni mwa wiki kwa kufungwa magoli mawili kwa moja na Atletico Madrid, na sasa vijana hao wa kocha Carlo Ancelotti wanaanza kibarua cha Kundi B dhidi Basel hapo kesho, wakati mahasimu wao Atletico wakisafiri kuanza shughuli ya kundi A dhidi ya Olympiakos Piraeus wa Ugiriki.
Washindi wa mwaka wa 2013 Bayern Munich nao wataanza safari ya kufika fainali ya Juni 6, 2015 itakayochezwa mjini Berlin, kwa kucheza mchuano wa Kundi E dhidi ya mabingwa wa Uingereza Manchester City siku ya Jumatano. Timu hizo mbili zinakutana katika awamu ya makundi kwa mara ya tatu katika kipindi cha miaka minne, kama tu itakavyokuwa kwa makamu bingwa wa Champions League mwaka wa 2013 Borussia Dortmund na Arsenal, ambao watafufua ushindani wao kesho katika Kundi D.
Schalke ambao wameanza msimu kwa kuyumbayumba, watacheza nyumbani dhidi ya Chelsea katika mechi ya Kundi G siku ya Jumatano, ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo kwa timu hizo kukutana.
Liverpool watakamilisha orodha ya wawakilishi wa Uingereza watakapowaalika Ludogorets katika mchuano wa Kundi B. Timu ya nne ya Ujerumani, Bayer Leverkusen itacheza ugenini dhidi ya Monacho katika kundi C.
Uhispania pia ina timu nne katika dimba hilo, ambapo Barcelona wataanzisha kundi F dhidi ya Apoel Nicosia, nao Athletic Bilbao watakwaruzana na Shakhtar Donestk katika kundi H.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu