1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SADC kufumbua kitandawili cha Zimbabwe

5 Novemba 2009

Mugabe na Tsvangirai suluhu leo ?

https://p.dw.com/p/KOyx
Robert Mugabe na Morgan Tsvangirai .Picha: picture alliance/dpa

Viongozi wa SADC-Jumuiya ya uiano na maendeleo kusini mwa Afrika, wamekusanyika leo mjini Maputo,Msumbiji kwa jaribio jengine la kumaliza mvutano katika serikali ya Zimbabwe iliogawanya madaraka kati ya chama cha rais Robert Mugabe (ZANUpf) na cha waziri-mkuu Morgan Tsvangirai (MDC).Hali ya mambo nchini inazidi kuwa mbaya na wapinzani kuzidi kuandamwa.

Rais Robert Mugabe na waziri-mkuu Morgan Tsvangirai , wameitwa Maputo na Jumuiya ya SADC kushauriana jinsi ya kujikomboa kutoka mvutano wao ulioibuka kiasi cha wiki 3 nyuma. SADC mdhamini wa mapatano hafifu ya umoja wa taifa inawakilishwa mkutanoni na mwenyekiti wake Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, rais wa Msumbiji Armando Guebuza,Rais Rupiah Banda wa Malawi,Jacob Zuma wa Afrika kusini na mfalme Mswati III wa Swaziland.Serikali ya muungano ya miezi 8 sasa ya Zimbabwe imekuwa ikiyumbayumba tangu chama cha Bw.Tsvangirai cha MDC , kujitoa kwa sehemu tu serikalini.

Serikali ya muungano ya Zimbabwe ya miezi 8 sasa, imekumbwa na msukosuko tangu chama cha Bw.Tsvangirai cha MDC kuamua kutohudhuria vikao vya baraza la mawaziri. Sababu ni kuwa kinalalamika kukataa chama cha Mugabe cha ZANUpf kugawana madaraka kikamilifu na kutekeleza mageuzi yalioafikiwa ndani ya mapatano .Hatahivyo, mawaziri wa chama cha MDC wanaendelea kushughulikia majukumu ya wizara zao.

Mashirika kadhaa yanayotetea haki za binadamu kwamba mzozano huu unaweza ukaitosa tena Zimbabwe katika machafuko ya kisiasa yaliogubika uchaguzi wa rais wa mwaka jana.Tayari hivi sasa, hali ni ya wasi wasi kwani wapinzani wa rais Mugabe, wanaendelea kuandamwa na hata wengine kutekwanyara.

Sydney Chisi, msemaji wa muungano unaotetea haki za kiraia "Crisis in Zimbabwe coalition" anapokea kila kukicha taarifa za kuandamwa wapinzani: Asubuhi ya jana tu ,anaripoti ,jaribio lilifanywa kumtekanyara Katibu-mkuu wa Shirika la wafanyikazi wa mashambani, Gertrude Hambari.Anasema,

"Hakuna ajuwae wazi , ni akina nani hao watekanyara.Huja kwa motokaa zisizo na nambari na hutimiza kazi yao kwa kasi kubwa.Ghafula, huondoka na mateka wao hata kabla majirani kutambua kilichotokea."

Kwa upande wake, rais Mugabe, anadai ametimiza sehemu yake ya makubaliano na anashikilia kuwa chama cha MDC, kifanye kampeni ya kuondoshewa chama cha ZANUpf vikwazo vilivyowekewa na nchi za magharibi. Pamoja na vikwazo hivyo, ni vizuwizi vya usafiri na misaada jumla ya fedha kwa Zimbabwe.

Hali ya wasi wasi katika serikali hii mpya ya Zimbabwe ilidhihirika mwezi uliopita pale bingwa wa haki za binadamu wa UM alipowekwa kizuizini Uwanja wa ndege wa Harare na maafisa wa usalama wa Zimbabwe ingawa alisema, alialikwa nchini na waziri mkuu Tsvangirai.

Shirika linalotetea haki za binadamu (HUMANRIGHTS WATCH ) limewataka viongozi wanaokusanyika leo Maputo wa Jumuiya ya SADC kukishinikiza chama cha Bw. Mugabe (ZANUpf) kukomesha kile ilichokiita, "maovu yanayoendelea ya kukiuka haki za binadamu" nchini Zimbabwe.

Mtayarishi:Ramadhan Ali/ RTRE

Uhariri: Abdul-Rahman