Saaid waziri mkuu mpya Somali
7 Oktoba 2012Wanadiplomasia wanamueleza waziri mkuu huyo mpya kuwa mtu ambaye hana doa kuhusiana na uhasama uliopo baina ya koo za nchi hiyo pamoja na uhasama ambao umeikumba Somalia kwa miongo kadha.
"Namfahamu Saaid na nimemteua kwasababu ana uwezo," amesema rais Mohamed , ambae pamoja na waziri wake huyo mkuu wanakabiliwa na kazi ngumu ya kujaribu kuunda serikali kuu ya kwanza itakayokuwa na uwezo , tangu kuzuka kwa vita vya ndani mwaka 1991.
Raia waombwa
"Nalitolea mwito bunge na raia kumuunga mkono," amesema katika taarifa.
Licha ya kuwa rais na waziri mkuu ni watu wapya katika kazi hizo, watakabiliwa na matatizo ambayo yalikuwapo kabla, ambayo ni siasa za kiukoo, rushwa iliyokithiri, uharamia baharini na wapiganaji wa kundi la Kiislamu.
Mogadishu sasa shwari
Mogadishu, mji mkuu ambao hadi mwaka jana ulikuwa umezingirwa na mapigano ya mitaani kati ya wanamgambo wa kundi la al-Shabaab wenye mafungamano na kundi la al-Qaeda na wanajeshi wa jeshi la umoja wa Afrika , sasa ni mji wenye shughuli za kimaendeleo, ambako majengo yenye alama za risasi taratibu yanafanyiwa ukarabati na kujengwa mapya.
Majeshi ya Umoja wa Afrika pia yamelisukuma kundi la al-Shabaab nje ya mji wa kusini wa bandari wa Kismayu wiki iliyopita, ikiwa ni ngome ya mwisho ya kundi hilo la wapiganaji , baada ya miaka mitano ya uasi, lakini serikali ya Somalia bado haina udhibiti katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na hali ya usalama bado inaendelea kuwa tete.
Wapiganaji wa al-Shabaab , ambao wanasema Saaid ni kibaraka wa mataifa ya nje, huenda wakashambulia kwa mabomu na kufanya vita vya chini kwa chini. Mshambuliaji wa kujitoa muhanga wa kundi la al-Shabaab alijiripua kiasi ya kilometa 30 kutoka Mogadishu, na kuwajeruhi wanajeshi wawili wa serikali.
Al-Shabaab wasema hawaelewi
"Waziri mkuu huyo mpya hana tofauti na wale waliokuwa kabla yake, wote wameletwa na mataifa ya magharibi", Sheikh Ali Mohamud Rage, msemaji wa al-Shabaab , ameliambia shirika la bahari la Reuters.
"hata ibadilisha Somalia.Tutapambana na kuendelea kuizuwia serikali hii ya makafiri."
Saaid amekuwa mfanayabiashara maarufu katika nchi jirani ya Kenya na amemuoa Asha Haji Elmi, ambaye ni mwanaharakati maarufu wa kupigania amani.
Mwanadiplomasia wa mataifa ya magharibi amesema kuwa Saaid ana sifa ya kuwa hana mahusiano na siasa za kiukoo za Somalia, sawa na rais mpya wa nchi hiyo, na taarifa za kuteuliwa kwake zitakaribishwa na serikali za mataifa ya kigeni.
Mohamud , msomi wa zamani na mwanasiasa mpya binafsi, alichaguliwa kuwa rais katika kura ya siri Septemba 10, hali iliyosifiwa na wafuasi wake kuwa ni kura ya mabadiliko.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga