1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saa chache zimebakia Trump kuapishwa

20 Januari 2017

Donald Trump atakuwa rais wa 45 wa Marekani amerejelea ahadi yake ya kampeni ya kuifanya nchi yake kuwa taifa lenye nguvu zaidi kuliko hapo awali, Hata hivyo maelfu waandamana nchini Marekani kupinga kuapishwa kwake.

https://p.dw.com/p/2W6H7
USA | Vorbereitungen für Trumps Inauguration in Washington
Picha: REUTERS/B. Snyder

Leo Ijumaa Donald Trump ataikamilisha safari yake ya kuingia katika ikulu ya Marekani ambapo atachukua hatamu za uongozi kutoka kwa Rais Barack Obama anayeondoka madarakani. Katika hotuba yake kabla ya kuapishwa jioni ya jana, Trump alisema kuwa yeye ni mtumishi wa harakati zenye lengo la kuleta mabadiliko nchini Marekani. Amewaahidi Wamarekani kwamba taifa hilo litabadilika. Bilionea huyo aliwaambia maalfu ya watu waliokuwa wanamshangilia mbele ya jengo la Kumbukumbu ya Rais Abraham Lincoln kwamba ataleta umoja miongoni mwa Wamarekani. Aliahidi kutimiza mambo ambayo hayajawahi kufanyika kwa miongo mingi.

Trump aliwasili Washington pamoja na mkewe, Melania, kwenye uwanja wa kijeshi wa Andrews na baada ya hapo msafara wake wa magari ulienda katika hoteli ya kimataifa ya Trump iliyopo karibu na ikulu kupata chakula pamoja na wabunge wa chama cha Republican, mawaziri wake watarajiwa na maafisa waandamizi.

USA | Trump-Familie am Lincoln Memorial anlässlich des "Make America Great Again Welcome Celebration concert"
Rais mteule wa Marekani Donald Trump na familia yakePicha: picture-alliance/CNP/AdMedia/C. Kleponis/

Hata hivyo Trump anatarajiwa kuapishwa wakati ambapo nchi yake imegawanyika vibaya. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni, ni asilimia 40 tu ya Wamarekani ndio wanamuunga mkono. Hata ambapo maalfu ya watu wanaomuunga mkono wanatarajiwa kumshamngilia bilionea huyo aliyejigeuza kuwa mtetezi wa maslahi ya tabaka la wafanyakazi, maalfu kwa maalfu ya Wamerakani wengine wanatarajiwa kwenda Washington kuzipinga sera zake wakati wa kuapishwa kwake.  Licha ya hayo makamu wa rais mteule, Mike Pence, amesisitiza kwamba Trump yupo tayari kuanza kazi:  Trump ataapishwa na Jaji Mkuu John Roberts wa Mahakama ya Juu ya Marekani. Marais watatu wa zamani pamoja na waheshimiwa wengine kadhaa, ikiwa pamoja na aliyekuwa mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi wa Novemba mwaka jana, Bi Hillary Clinton, watahudhuria hafla ya kuapishwa kwa Trump. Lakini thuluthi moja ya wabunge wa chama cha Democratic wataisusia hafla hiyo. Maalfu ya  wapinzani wa Trump waliandamana jana mjini New York wakiwemo wacheza filamu maarufu Robert  de Niro, Alec Baldwin na muongoza filamu mshindi wa tuzo ya Oscar, Michael Moore, wakipinga siasa za Trump kuelekea wahamiaji, Waislamu na huduma za afya na kijamii.  

Kilele cha shughuli za leo kitafikiwa kwa hotuba ya Trump kwa Wamarekani, mara baada ya kula kiapo cha kuingia madarakani. Msemaji wake, Sean Spicer, amesema kwamba hotuba yake ya kuingia ikulu haitakuwa juu ya ajenda anazotaka kuzitekeleza, bali zaidi itakuwa ya kifalsafa jinsi anavyoiona Marekani. Spicer pia amesemaTrump yupo tayari kuzitekeleza sera zake mara tu atakapoanza kazi ikiwa pamoja na kutia saini hati zinazohusu huduma ya afya, ugaidi na uhamiaji.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/DPAE/http://dw.com/p/2W5mD
Mhariri: Mohammed Khelef