1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saa 48 za kusitisha mapigano zamalizika nchini Yemen

22 Novemba 2016

Kundi la waasi wa Houthi na vikosi vya serikali vyalaumiana kukiuka makubaliano baada ya saa 48 za kusitisha mapigano kumalizika nchini Yemen.  Zaidi ya watu 7000 wameuwawa hadi kufikia sasa.

https://p.dw.com/p/2T3HA
Jemen Zerstörung
Picha: Reuters/A.Mahyoub

Kwa mujibu wa msemaji wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia Ahmed Assiri, Muda wa makubaliano hayo ya muda mfupi ya kusimamishwa mapigano umemalizika na kwamba hautaongezwa.  Assiri amesema waasi wa Kishia wa Houthi muda mfupi tu baada ya kuanza makubaliano hayo, waliyakiuka mara 113  katika miji ya Najran na Jizan iliyopo katika mpaka wa Yemen na Saudi Arabia.  Msemaji huyo wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia amesema kuwa waasi wa Houthi hawakuheshimu makubaliano hayo. Watu zaidi wameuwawa katika mji wa Taez ulio Kusini Magharibi mwa Yemen kutokana na mashambulio ya makombora na hali ya usalama katika eneo hilo si nzuri. Msemaji wa jeshi la muunganounaoongozwa na Saudi Arabia Ahmed Assiri ameeleza kuwa waasi wa Houthi wamekiuka zaidi ya makubaliano 500 tangu yalipoanzishwa na kwamba asilimia 80 ya ukiukaji huo umetoea ndani ya Yemen.

Kwa upande wake waasi wa Houthi wanakilaumu kikosi cha jeshi la Yemen kinachosaidiwa na Saudi Arabia kwa kukiuka mara 114 makubaliano ya kusitisha vita ndani ya saa 48 tangu kuanza kwa makubaliano hayo, wamesema ndege za kivita za Saudi Arabia zilipiga kwa mabomu kambi inayosimamiwa na waasi hao katika mji mkuu wa Sanaa.  Msemaji wa kikosi cha  waasi wa Houthi Sharaf Loqman aliliambia shirika la habari linalowaunga mkono la Saba kwamba jeshi la Yemen lilikiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.  Jeshi hilo likisaidiwa na Saudi Arabia lilishambulia kwa roketi  baadhi ya miji iliyo mpakani na liliendesha operesheni ya kuwakamata raia ndani ya muda uliotakiwa kusitisha mapambano.

Jemen Protest UN Bürgerinitiative
Wanawake wa Yemen waonyesha jinsi vita vinavyochangia utapiamloPicha: picture alliance/Yahya Arhab/E

Nchi ya Yemen imekabiliwa na mapigano tangu mwaka 2014 wakati ambapo waasi wa Houthi waliuteka mji mkuu wa Sanaa hatua mabayo ilimlazimisha rais wa nchi hiyo Abd Rabbo Mansour kukimbilia katika mji wa kusini wa Aden na baadae alikwenda Riyadh, Saudi Arabia.  Machafuko yalizidi nchini humo kufikia mwezi Machi mwaka 2015 wakati ndege za kivita zilizoongozwa na jeshi la Saudi Arabia ziliposhambulia kwa mabomu maeneo yaliyokuwa yanashikiliwa na waasi wa Houthi.

Takriban watu 7000 wameshakufa kutokana na mapigano hayo huku zaidi ya watu 36,000 wakiwa wamejeruhiwa.  Shirika la watoto la Umoja wa Mataaifa UNICEF limetoa taarifa kwamba karibia watu milioni 3 wanahitaji misaada ya chakula kwa haraka.  Taarifa hiyo imeeleza kuwa watu milioni 1.5 wanakabiliwa na utapiamlo.

Mwandishi Zainab Aziz/ 

Mhariri:Yusuf Saumu