1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yafuta mkutano na waziri wa nje wa Ubelgiji

21 Septemba 2021

Rwanda imesema imeufuta mkutano uliopangwa kufanyika na waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Sophie Wilmes katika Umoja wa Mataifa, baada ya waziri huyo kuikosoa kesi dhidi ya Paul Rusesabagina ambaye ni raia wa Ubelgiji.

https://p.dw.com/p/40c2Y
Belgien I Außenministerin Sophie Wilmes
Picha: Jean-Christophe Verhaegen/AP/picture-alliance

Mnamo Jumatatu Rusesabagina aliyepata sifa kwa kuyanusuru maisha ya zaidi ya watu 1,200 wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ya Rwanda alihukumiwa kifungo cha miaka 25 jela na mahakama kuu ya nchi hiyo kwa kuhusishwa na ugaidi.

Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Wilmes amesema kwamba licha ya kutolewa mwito mara kadhaa na serikali yake mjini Brussels, Rusesabagina hakutendewa haki katika kesi iliyomkabili na hasa kuelekea haki ya kujitetea.

Aidha amesema hata sheria ya msingi ya kutomtia mtu hatiani kabla ya ushahidi kuthibitishwa haikuheshimiwa na kwamba masuala hayo yanaibua maswali kuhusu kesi hiyo na hukumu yake.

Familia ya Rusesabagina ambayo imekuwa ikiendeleza kampeni kimataifa ya kutaka aachiliwe huru, inahofia kwamba huenda akafia jela.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW