1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda kuwashitaki Wafaransa 20 kwa mauaji ya maangamizi

Isaac Gamba
30 Novemba 2016

Serikali ya Rwanda imeanzisha uchunguzi dhidi ya maafisa 20 wa Ufaransa wanaoshukiwa kwa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994, hatua ambayo inaashiria kuzidisha uhasama kati  ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/2TVcw
Symbolbild - Ruanda Opfer des Bürgerkriegs
Picha: Getty Images/C. Somodeville

Mwendeshaji mkuu wa mashtaka wa Rwanda, Richard Muhumuza, anasema kwa sasa uchunguzi wao unawamulika watu 20, wanaotakiwa kutoa maelezo kwa maafisa au kujitetea kuhusu madai dhidi yao. "Ushirikiano wao utawasaidia waendesha mashtaka kuamua iwapo Wafaransa hao watafunguliwa mashtaka au la", alisema.

Ufaransa inashutumiwa kwa kupuuza au kukosa kugundua ishara za kutokea mauaji hayo, huku ikiendelea kuwapa mafunzo wanajeshi na wapiganaji wanaotuhumiwa kufanya mauaji.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Rwanda na Ufaransa umezorota katika siku za hivi karibuni, baada ya Ufaransa kufungua tena uchunguzi kuhusu kudunguliwa kwa ndege iliyomuuwa rais wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, ambao wengine wanadhani unamlenga Rais Paul Kagame na chama chake cha RPF.