Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema Rwanda ina kila sababu ya kuwahifadhi wanafunzi hao, huku baadhi ya wananchi wa kawaida wakisema huenda wanafunzi hao wakawa mzigo.
Ndege iliyowaleta wanafunzi wa Chuo cha Uongozi cha Afghanistan, SOLA kwa ufupi, wafanyakazi wa chuo hicho pamoja na familia zao, iliondoka mjini Kabul wiki iliyopita, wote wakifikia 250.
Taarifa zinaarifu kwamba wataendelea na masomo yao nchini Rwanda kwa muda wa muhula mmoja, kama alivyoeleza rais wa chuo hicho, Shabana Basij-Rasikh kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Bi Yolande Makolo, ameiambia DW kwamba Rwanda iko tayari kuwapokea wananchi hao wa kigeni huku akijizuia kutoa taarifa zaidi.
Amesema “Kama ilivyotangazwa hapo awali na Wizara ya Elimu, Rwanda itawapokea jamii hiyo ya SOLA. Hata hivyo, tunaheshimu ombi lao la maisha yao binafsi kutotangazwa na kwa maana hiyo sina la ziada kwa sasa.”
Wachambuzi wa masuala ya mambo na raia wanasemaje?
Bwana John Mugabo ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa mkazi wa Mji wa Kigali. Amesema Rwanda inatakiwa kuwapokea wanafunzi hao kulingana na Mkataba wa Geneva juu ya Sheria za Kibinadamu ambao huwapa waathirika wa vita haki ya kukimbia na kupokelewa na nchi zenye usalama.
Lakini pia, kama anavyoeleza, Rwanda kama nchi ambayo kimataifa inatambulika kwa kuwaendeleza wanawake na kuwaweka katika nyadhifa za uongozi ambapo ndio wengi bungeni na hata katika baraza la mawaziri, ina kila sababu ya kuwahifadhi wanafunzi hao wa Afghanistan hasa ukizingatia ni wa kike.
Ukiongea na wananchi wa kawaida, baadhi wanaipongeza serikali kwa kukubali kuwapokea wageni hao huku wengine wakijiuliza kama Rwanda imejiandaa ipasavyo.
Mmoja ya raia wa Rwanda aliyejitambulisha kwa jina la Vital amesmea “Waafghanistan tunawakaribisha, wanyarwanda ni watu ambao wanapenda watu bila kujali asili yao”
Hata hivyo mwingine aliyejitambulisha kama Jonathan amesema "Najiuliza kama Rwanda ina uchumi wa kutosha wa kuwatunza wageni na wenyeji sababu uchumbi unayumbayumba leo hii kutokana na athari za Covid-19. Wapo wanyarwanda wengi ambao wanalia wakiomba serikali misaada na serikali haiwasaidii vya kutosha.”
Kwa sasa, Rwanda imewahifadhi wakimbizi laki moja na elfu arobaini na tisa, ambao wengi wao ni kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.