Rwanda kufanya upimaji mkubwa wa virusi vya corona shuleni
17 Novemba 2020Wizara za elimu na afya zimesema kwamba zoezi hili litafanyika kwa awamu na litazihusisha shule zote za msingi, sekondari na vyuo vikuu hasa kwenye maeneo ya nchi ambayo tayari yanaonekana kuwa na kiasi kikubwa cha maambukizi ya covid-19.
Awamu hii ya kwanza itahusu kuchukua sampuli za wanafunzi elfu 2,500 wa shule za msingi mjini Kigali, sampuli za wanafunzi 2,000 wa shule za sekondari mjini na sampuli 500 za wanafunzi wa vyuo vikuu kadhalika mjini Kigali na baadaye litaendelea nchi nzima
Ni zoezi ambalo limeanza wiki mbili baada ya awamu ya kwanza ya shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu hasa wale waliokuwa wanakaribia kufanya mitihani yao ya mwisho wakati ulipozuka ugonjwa wa corona. Waziri wa elimu Dr Uwamaliya Valentine amesema kwamba zoezi hili halitaathiri mchakato mzima wa masomo kwa sababu linafanyika kwa tahadhari kubwa
"Kinachotarajiwa siyo kufunga shule zote nchini, isipokuwa tutajikita pale tutakapokuta kuna tatizo ndipo tutakapotilia mkazo na ndiyo maana kwa kila shule tumeandaa chumba cha dharura", alisema waziri wa elimu.
Kwa shule ambazo tayari zimeshafunguliwa wanafunzi na walimu wao wamesema tahadhari inaendelea kwa kiwango cha juu. Wizara afya inashikilia kwamba zoezi hili pia linalenga kufanya utafiti wa picha ya jinsi ugonjwa huo ulivyo mashuleni. Dr Sabin Nsanzimana ni mkurugenzi mkuu wa taasisi ya tiba nchini
"Kwa siku hizi tunaona idadi ya maambukizi ikishuka, lakini kushuka kwa maambukizi hakuna maana kwamba virusi vimeisha, hapana isipokuwa tunaendelea kufanya utafiti ili kujua hata kule ambako vitakuwa vimejifisha bila sisi kujua na ukipata maeneo walipo watu wengi lakini uchukue nafasi hiyo kujua hali ikoje", amesema Dr Sabin.
Mpaka sasa watu 45 wameshafariki nchini Rwanda kutokana na ugonjwa wa corona huku maambukizi yakifikia watu 5,491 na waliopona wakiwa ni watu 5,004 huku wengine 442 wakiendelea kuuguzwa mahospitali.