1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda imetetea mkataba wake wa kuidhamini Arsenal

27 Juni 2018

Jarida la Uingereza la Mail toleo la Jumapili limesema Rwanda imeilipa klabu hiyo ya London pauni milioni 30, ili wachezaji wa klabu hiyo ya Arsenal wavae jezi zilizoandikwa "Tembelea Rwanda"

https://p.dw.com/p/30NWF
Fußball, Europa League, Arsenal London vs 1. FC Köln
Picha: picturealliance/Citypress24/S. Bowen

Rwanda imeukingia kifua mkataba wake wa mabilioni ya fedha kuidhamini timu ya soka ya Uingereza, Arsenal, na kuwaambia wanasiasa wa mataifa yanayotoa ufadhili ya Ulaya kwamba hilo si jukumu lao.

Jarida la Uingereza la Mail toleo la Jumapili limesema Rwanda imeilipa klabu hiyo ya London pauni milioni 30, ili wachezaji wa klabu hiyo ya Arsenal wavae jezi zilizoandikwa "Tembelea Rwanda" ambayo ni alama ya utalii itakayokuwa kwenye mkono mmoja wa jezi.

Baadhi ya wanasiasa wa Uingereza, Uholanzi na mataifa mengine wafadhili wamekosoa uamuzi huo uliochukuliwa na taifa la Afrika ambalo kulingana na benki ya dunia, lilipata zaidi ya dola bilioni 1, ya misaada kutoka nje na misaada ya kimaendeleo kwa mwaka 2016, kuifadhili timu hiyo inayopendwa na Rais Paul Kagame.

Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba, aliwajibu wabunge hao wa Uingereza kwamba fedha hizo zilitokana na mapato ya utalii, na si za misaada, hivyo suala hilo haliwahusu.