Rwanda: Congo yakiuka usalama wa anga
29 Desemba 2022Rwanda inasema hayo wakati kukiwa na mzozo unaotokota kati ya nchi hizo mbili jirani kuhusiana na waasi wanaoendesha harakati zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Serikali ya Rwanda imesema katika taarifa kuwa ndege ya kivita aina ya Sukhoi-25 kutoka Congo iliingia katika anga ya Rwanda kwenye Ziwa Kivu katika Mkoa wa Magharibi wa Rwanda jana mchana kabla ya kurejea mara moja nchini Congo. Tukio hilo linajiri chini ya miezi miwili baada ya Kigali kutuhumu ndege nyingine ya kivita ya Congo kwa kukiuka anga yake. Rwanda imesema uchokozi huo lazima ukomeshwe. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaituhumu Rwanda kwa kuliunga mkono kundi la waasi wa M23, ambalo limekamata maeneo ya nchi kutoka kwa wanajeshi wa Congo na wapiganaji washirika katika miezi ya karibuni. Kigali inakanusha tuhuma hizo, ambazo pia zinaungwa mkono na wataalamu wa Umoja wa Mataifa pamoja na Maerekani, Ufaransa na Ubelgiji.