1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto: Kenya iko kwenye mkondo mzuri

9 Novemba 2023

Rais William Ruto wa Kenya amezitetea sera za serikali ya Kenya Kwanza wakati wa hotuba yake ya kwanza rasmi kwa taifa. Ruto ameitoa hotuba hiyo bungeni katika kikao cha pamoja cha maseneta na wabunge.

https://p.dw.com/p/4YcjZ
Rais wa Kenya William Ruto
Rais wa Kenya William RutoPicha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Hotuba ya rais inajiri katika wakati ambao wakenya wanalalamikia hali ngumu na gharama ya maisha iliyoongezeka baada ya kupandishwa kodi. Ifahamike kuwa ni kiongozi mmoja pekee wa upinzani wa chama cha Wiper Democratic, Kalonzo Musyoka aliyehudhuria kikao cha leo.

Muda mfupi baada ya saa nane u nusu alasiri, Rais William Ruto alikagua gwaride la heshima nje ya majengo ya bunge kabla ya nyimbo za taifa na jumuiya ya afrika mashariki kupigwa kuashiria ufunguzi wa kikao.

Alipopanda jukwaani, Rais Ruto alizitetea vikali sera za serikali ya Kenya Kwanza na kushikilia kuwa taifa liko kwenye mkondo mzuri.

Soma pia: Kenya: Mfumo wa elimu na mtihani wa 8-4-4 wafikia kikomo 

Serikali ya Kenya Kwanza imekuwa ikinyoshewa kidole cha lawama kwa ongezeko la gharama za maisha na bei za bidhaa kwa jumla. Ifahamike kuwa Kenya ina deni la umma la dola bilioni 2 za Marekani ambalo linatakiwa kulipwa mwaka ujao.

Kwenye hotuba yake Rais William Ruto ameahidi kuwa deni la hati za dhamana za Eurobond la shilingi bilioni 500 za Kikenya litalipwa ifikapo mwezi ujao wa Disemba.

Wakenya wamekuwa wakilalamika kutokana na kuongezeka kwa gharama kubwa ya maisha
Wakenya wamekuwa wakilalamika kutokana na kuongezeka kwa gharama kubwa ya maishaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Hotuba ya rais iligusia pia masuala ya usalama likiwemo la kupeleka kikosi cha polisi nchini Haiti, mjadala unaozua mitazamo tofauti.

Hii leo Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alisema Kenya haitapeleka polisi wake Haiti hadi pale mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa yakaporidhia kutoa fedha za kufadhili shughuli za ujumbe huo wa kulinda amani utakaojumuisha pia nchi nyingine kadhaa.

Suala la ongezeko la gharama za maisha, Rais Ruto amesisitiza kuwa mpango wa kugawa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima umeanza kuzaa matunda kwani bei ya unga wa mahindi tayari imeshuka kwa hadi shilingi 250 kwa mfuko wa kilo mbili.

Soma pia: Mahakama Kenya yaongeza amri ya kuzuia polisi kupelekwa Haiti

William Ruto ameelezea kuwa madhila ya UVIKO 19, ukame na siasa za dunia yameathiri uchumi wa taifa kwa kiasi kikubwa. Baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao hicho wana mtazamo tofauti. Mbunge wa Bumula Anami Wamboka anadai kuwa ahadi ni nyingi kuliko vitendo.

Kauli hizo zinaungwa mkono na mbunge wa Budalangi Raphael Wanjala anayesisitiza kuwa suala la ajira bado ni donda ndugu.

Hotuba hii ni ya kwanza rasmi ya Rais William Ruto tangu kushika hatamu miezi 14 iliyopita.