1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto azungumzia mabadiliko ya katiba

8 Februari 2019

Makamu wa rais wa Kenya, William Ruto ameelezea kuhusu miito ya kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba nchini Kenya huku akitoa mapendekezo kadhaa yanayoweza kuzikabili changamoto hizo.

https://p.dw.com/p/3D1Wn
Kenia Präsident William Ruto beim Eco Forum Global Annual Conference in China
Picha: Imago/Xinhua

Makamu wa rais wa Kenya, William Ruto ameelezea kuhusu miito ya kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba nchini Kenya kufuatia changamoto mbalimbali na hususan zinazozikabili serikali za kaunti huku akitoa mapendekezo kadhaa yanayoweza kuzikabili changamoto hizo. Aidha ameelezea utayari wake wa kujibu tuhuma za rushwa zinazomkabili, huku akisema chama cha Jubilee kinaangazia zaidi kutekeleza ahadi zake kwa wananchi, na si uchaguzi ujao wa 2022. 

Makamu wa rais Ruto alizungumzia namna mabadiliko hayo ya 2010 ya katiba yalivyoibadilisha Kenya, akiwa katika taasisi ya Chatham House jijini London.

Amesema pamoja na masuala mengine mambo yaliyofikiwa kutokana na mabadiliko hayo, ni pamoja na kuwezesha kuitenganisha mamlaka na bunge ili kuzifanya taasisi hizo kufanya kazi kazi bila ya kuingiliwa, uwazi kwenye bajeti hivyo kuondoa sintofahamu ya mipango na matumizi, kwa kuuhusisha umma na bunge kufanya maamuzi. Lakini pia, uhuru wa taasisi hiyo umewafanya wabunge kupitisha kwa urahisi miswada takriban 290 kwa miaka 7 iliyopita, ikilinganishwa na 83 ya muda kama huo, kipindi cha nyuma.

Kenia Uhuru Kenyatta  William Ruto
Rais Uhuru Kenyatta akiwa na makamu wake William RutoPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Amegusia pia mafanikio kwenye sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na yaliyofikiwa kupitia mpango wa kugawa madaraka, ambayo ni pamoja na mgawo wa bajeti na utekelezaji wa miradi kupitia bajeti hizo kwenye serikali za kaunti, ingawa amekiri bado kuna changamoto kadhaa ambazo ndizo zimechangia kuongezeka kwa miito ya kufanyika kwa marekebisho ya katiba.

Kufuatia hatua hiyo, Rutto ametoa mapendekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na wagombea wa urais kuingia moja kwa moja kwenye bunge la kitaifa.

"Bunge la kitaifa linatakiwa kuwa na muundo mpya ili kuwa na baraza la mawaziri linaloongozwa na rais na kambi ramsi ya upinzani inayoongozwa na kiongozi wa chama au muungano wa vyama ambaye mgombea wake wa urais alipata nafasi ya pili kwenye uchaguzi. kiongozi wa chama kilichokuwa cha pili anakuwa kiongozi wa upinzani na yeye na mgombea mwenzake wanakuwa moja kwa moja wabunge na wanachukua jukumu la kuwa upinzani rasmi."

Kenia William Ruto
Ruto anakabiliwa na tuhuma za rushwa, na amesema yuko tayari kuzijibu iwapo zitatolewa kwa mfumo rasmi.Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Asema yuko tayari kujibu tuhuma za rushwa.

Aidha Ruto Amezungumzia pia madai ya rushwa yaliyotolewa dhidi yake na aliyekuwa naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee, David Muradhe, akisema hataweza kumjibu kwa kuwa hafai kupata majibu kutoka kwake, ingawa alisisitiza kwamba yuko tayari kuzijibu tuhuma zinazotolewa dhidi yake.

"Niko tayari kujibu tuhuma zozote za rushwa dhidi yangu. Uamuzi wa nani atasimama kama mgombea wa Jubilee, 2022 sio wa mtu binafsi, wa si wa watu wachache, utakuwa ni uamuzi wa chama cha Jubilee, chini ya uongozi wa rais Uhuru Kenyatta, na wanachama wataamua nani atakuwa mgombea. Kwa sasa hatuzingatii nani atakuwa mgombea, kwa sasa tunaangalia tunafanyaje kutekeleza ahadi tulizitoa kwa raia wa Kenya, na utekelezaji wa manifesto ya Kenya, hilo ndilo ninaloangazia."

Kuhusu suala la wakimbizi, amesema hatua kubwa zimepigwa tangu kuliposainiwa makubaliano kati ya Kenya, Umoja wa Mataifa na Somalia ya kuwarejea kwa hiyari wakimbizi hao nchini Somalia, na ameshuhudia hilo wakati alipotembelea kambi ya Dadaab miezi minne iliyopita. Takriban wakimbizi 100,000 ya wakimbizi wamerejea makwao kufuatia kurejea kwa hali ya utulivu nchini humo chini ya ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini humo, AMISOM.

Akizungumzia suala la Wakenya waishio nje, kufuatia swali juu ya namna Kenya inavyowachukulia raia hao, amekiri kwamba pamoja na kutambua mchango wao mkubwa lakini bado hawajaweza kuwafikia kikamilifu. Hata hivyo amewahakikishia kuhusu juhudi kadhaa zinazofanyika ili kuweza kulitambua kundi hilo muhimu linaloishi nje ya Kenya.

Mwandishi: Lilian Mtono

Mhariri: Yusuf Saumu