Ruto aitisha maandamano ili kukabiliana na upinzani
17 Julai 2023Kwenye mkutano uliofanyika ikulu, rais amesema kuwa mandamano ya kila juma yanayofanywa na upinzani yamechukua mwelekeo wa kisiasa baadala ya kuangazia gharama ya maisha.
Kwenye mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa juma katika ikulu ya Nairobi na kuhudhuriwa na zaidi ya viongozi 200 wa kambi ya Kenya Kwanza, Rais Ruto alionyesha kutamaushwa kwake na jinsi maandamanohayo yamekuwa yakifanyika licha ya kuwepo kwa asasi za kuyadhibiti.
Wabunge waliohudhuria mkutano huo walitaka kufahamu utendji kazi wa Mkuu wa Huduma ya Ujasusi, Noordin Haji, na Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome, wakisema kuwa idara hizo zimeonekana kulegea mara si moja kwenye maandamano hayo ambayo huongozwa na kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga.
Hadi kufikia sasa watu 10 wameshauawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, huku 300 wakitiwa nguvuni kwenye vurugu za maandamano hayo.
Soma pia:Watu 6 wauawa katika maandamano ya upinzani Kenya
Aidha mali ya thamani ya shilingi bilioni tatu imeharibiwa.
Rais Ruto ameuonya vikali upinzani kwa kulapa kwamba maandamano kamwe hayawezi kushuhudiwa katika taifa hilo la Afrika mashariki.
"hayo maandamano hayawezi kufanyika, mtu huyu alileta fujo, akajaribu mapinduzi na watu wakauwawa."
Alisema rais Ruto ambae amekuwa akitupiwa lawama na upinzani na waandamanaji kutoshughulikia tatizo la kupanda kwa gharama za maisha.
"Kwa sasa tunalipa deni la alilolisababisha na bado anaendelea kuleta fujo."
Ukosoaji dhidi ya Raila waongezeka
Kwenye taarifa yao kwa vyombo vya habari, Kiongozi wa wengi katika bunge la Taifa, Kimani Ichungwa, na mwenzake wa Seneti, Aaron Cheruiyot, wamemkosoa Raila kwa kuendeleza kampeni ya maandamano kote nchini.
Taarifa hiyo imesema kuwa Raila analipiza kwa kuwa alishindwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Imeongeza kusema kuwa Raila anapanga kuingia kwenye serikali kupitia mlango wa nyuma.
Lakini kwa upande wake, kiongozi huyo mkongwe wa upinzani amesema kuwa maandamano ya sasa yanalenga kukabiliana na uongozi wa kiimla, ufiisadi na ujanja.
Soma pia:Maandamano ya upinzani yaendelea kuiandama Kenya
Aidha ametaja kuwa licha ya maafa dhidi ya wafuasi wa Azimio, Wakenya hawajawahi kupoteza kwenye vita vya ukombozi.
"Tumesema siku ya Jumatano, mpo tayaarii" Raila aliwauliza wafuasi wake huku wakimshangiria kuonesha wanakubaliana na hoja za kiongozi huyo mwenye ushawishi mkubwa miongoni mwa wakenya.
"Sisi si majambazi, si wale tunataka ugomvi, tunafanya kila kitu kwa sababu" Aliwaambia wafuasi hao ambao wengi miongoni mwao ni vijana.
UN yalaani matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji Kenya
Ubalozi wa Kudumu wa Kenya katika Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa huko Geneva yamelaani matumizi ya nguvu kupita kiasi ya polisi dhidi ya waandamanaji.
Kwenye taarifa iliyotolewa nao, wamezitaka mamlaka kuhakikisha kuwa Wakenyawanaruhusiwa kutumia hakizao kwa mujibu wa Kifungu cha 37 cha Katiba, na kuomba mamlaka husika kusitisha matumizi ya risasi za moto kuwatawanya waandamanaji.
Wakati hayo yakiarifiwa, Rais wa zamani Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wameshtakiwa kuhusu maandamano.
Soma pia:Amnesty International yailaumu Kenya uvunjifu haki za binaadamu
Martin Gitau, raia wa kawaida kutoka mjini Nairobi anataka viongozi hao wawajibishwe kwa uharibifu na madhara yaliyotokea wakati wa maandamano. Pia anaiomba mahakama kutoa amri ya kuwazuia kutangaza maandamano.
Rais Ruto amenukuliwa akidai kuwa Rais Mstaafu Uhuru ndiye anayefadhili maandamano hayo.
Kwa sasa, inasubiriwa kuona hatua atakayoichukuwa Rais Ruto baada ya kusema kuwa maandamano mengine hayatafanyika nchini.