Rusesabagina amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kutokana na kukutikana na hatia ya makossa ya Ugaidi. Amehukumiwa sambamba na aliyekuwa msemaji wa kundi lake aliyejulikana kama Callixte Sankara.
Jaji amesema Paul Rusesababgina, kiongozi mkuu wa kundi la FNL ambalo lilikuwa ni tawi la kijeshi la chama chake Paul Rusesabagina amekutikana na hatia ya ugaidi kwa kusaidia kuunda kikosi cha ugaidi kilichofanya mauaji ya raia wasio na hatia nchini Rwanda.
Soma pia: Mtoto wa Rusesabagina akosoa hukumu ya baba yake
Kesi ya Paul Rusesabagina imewashikirikisha pia washukiwa wengine 20 akiwemo aliyekuwa msemaji wa chama chake maarufu kama Callixte Sankara ambaye pia amehukumiwa kwenda jela.
Mahakama imefafanua kwamba mashtaka kuhusu mauaji yaliyofanyika katika maeneo ya Kitabi wilayani Nyamagabe kusini mwa Rwanda lenyewe linawahusu hata wale ambao hawakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mauaji dhidi ya raia kwa sababu hata wao walikuwa kwenye kundi hilo hata kama hawakuhusika katika mauaji hayo.
Wadadisi wa masuala ya kisheria wanasema kwamba hukumu hii haikuja kama mshangao kwa sababu kadhaa.
Paul Rusesabagina aliyejulikana sana ulimwenguni kupitia filamu yake ya Hotel Rwanda iliyohusu nafasi yake katika kusaidia maisha ya watu zaidi ya elfu moja aligeuka kuwa hasimu mkuu wa serikali baada ya kuunda kundi la wapiganaji na yeye mwenyewe kutangaza azma ya kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya Rwanda.
Sikiliza pia Uchambuzi kuhusu hukumu dhidi ya Rusesabagina:
Wakati wa kusoma hukumu hii Rusesabagina pamoja na mawakili wake hakuna aliyeonekana mahakamani na hii ni baada ya kususia kufika tena mahakamani tangu tarehe 12 mwezi Machi mwaka huu akisema kwamba alikuwa ni raia wa Ubelgiji na hivyo mahamakama za Rwanda hazikuwa na mamlaka ya kuendesha kesi yake.
Upande wa mahakama ulishikilia kwamba ulikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa sababu Paul Rusesabagina ni raia wa kuzaliwa wa Rwanda na kuhoji ikiwa raia wa Rwanda kwa nini aliamua kutangaza vita dhidi ya Rwanda na kufanya mauaji dhidi ya raia.
Haijulikana kama atakata rufaa kutokana kwamba yeye na mawakili wake hawakufika mahakama hii leo.