1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rubani wa Jordan atekwa na IS

Mjahida24 Desemba 2014

Jeshi la Jordan limethibitisha leo kwamba mmoja ya marubani wake ametekwa na kundi la wanamgambo wanaojiita Dola la Kiislamu, IS, baada ya ndege ya rubani huyo kuanguka nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1E9nu
Wanamgambo wa IS na rubani wa Jordan waliomteka
Wanamgambo wa IS na rubani wa Jordan waliomtekaPicha: picture-alliance/AP Photo/Raqqa Media Center of the Islamic State group

Shirika rasmi la habari la Jordan, Petra, linasema ndege ya jeshi la nchi hiyo ilianguka asubuhi ya leo ikiwa kwenye operesheni za kawaida kwenye eneo linalodhibitiwa na wapiganaji wa IS na kwamba rubani wa ndege hiyo sasa yumo mikononi mwa kundi hilo lenye siasa kali.

“Moja ya ndege zetu za kivita imeanguka, na rubani kuchukuliwa mateka Kundi la IS na wale wanaoliunga mkono ndio watakaowajibika kwa usalama wa rubani.” alisema afisa mmoja wa jeshi la Jordan aliyenukuliwa na shirika la habari la Petra.

Hata hivyo jenerali huyo hakutoa sababu ya kuanguka kwa ndege hiyo lakini IS pamoja na kundi la uangalizi nchini Syria wanasema ndege hiyo ya kijeshi ilidunguliwa na kombora la wanamgambo kutoka angani, karibu na mji wa kaskazini wa Raqaa nchini Syria.

Baadhi ya wanachama wa kundi la dola la Kiislamu
Baadhi ya wanachama wa kundi la dola la KiislamuPicha: Reuters/Stringer

Kundi la IS limetoa picha zinazomuonesha rubani huyo, Luteni Maaz al-Kassasbeh aliye na miaka 26, akiwa kifua wazi na aliyejaa maji baada ya kutolewa ziwani palipoanguka ndege yake.

Picha nyengine ilimuonesha rubani huyo akiwa amezungukwa na wapiganaji wa IS waliofunika nyuso zao. Ripoti zinasema wanamgambo huo wanaendelea kuchunguza eneo hilo kuona iwapo watampata rubani mwengine.

Baba wa kijana aliyechukuliwa Mateka aomba IS imuachie mwanawe

Naye baba wa mateka huyo anayejulikana kama Youssef alinukuliwa na vyombo vya habari vya Jordan akisema familia yake ilijulishwa juu ya kisa hicho na jeshi la anga nchini humo.

"Mtoto wangu mwengine alikutana na kamanda wa jeshi la angani la Jordan aliyemthibitishia kuwa mtoto wangu Maaz ametekwa na wanamgambo wa IS," alisema Youssef, akiwaomba wapiganaji hao kuonesha huruma na kumuachia mwanawe aliyehudumu ndani ya jeshi hilo kwa takribani miaka sita.

Youssef amesema ameambiwa na jeshi kuwa linajitahidi kuokoa maisha ya mwanawe na kwamba kiongozi wa nchi hiyo Mfalme Abdulla wa Pili pia amejihusisha katika shughuli za kumuokoa Luteni Maaz al-Kassasbeh.

Kiongozi wa Jordan Mwanamfalme Abdulla wa pili akiwa pamoja na rais wa Marekani Barrack Obama
Kiongozi wa Jordan Mwanamfalme Abdulla wa pili akiwa pamoja na rais wa Marekani Barrack ObamaPicha: Getty Images/Kevin Dietsch-Pool

Hili ni tukio la kwanza la mwanajeshi wa kigeni kutekwa au kuzuiliwa na wanamgambo wa Dola la Kiislamu, tangu muungano unaoongozwa na Marekani ulipoanzisha mashambulizi yake ya angani dhidi ya kundi hilo tarehe 23 mwezi wa Septemba.

Saudi Arabia, Jordan, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu, ni miongoni mwa mataifa ya Ghuba yanayoshiriki katika mapambano hayo, huku Qatar ikisaidia katika masuala ya kimkakati.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef