1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rowhani aongoza uchaguzi wa Iran

15 Juni 2013

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais wa Iran yanaonesha kuwa ulamaa mwenye msimamo wa wastani, Hassan Rowhani, anaongoza.

https://p.dw.com/p/18qO4
Iranian presidential candidate Hassan Rohani (L) waves to supporters in the central Iranian city of Shiraz June 11, 2013. Picture taken June 11, 2013. REUTERS/Fars News/Mohammad Hadi Khosravi (IRAN - Tags: POLITICS ELECTIONS) ATTENTION EDITORS - THIS IMAGE WAS PROVIDED BY A THIRD PARTY. FOR EDITORIAL USE ONLY. NOT FOR SALE FOR MARKETING OR ADVERTISING CAMPAIGNS. THIS PICTURE IS DISTRIBUTED EXACTLY AS RECEIVED BY REUTERS, AS A SERVICE TO CLIENTS
Wahlen im IranPicha: Reuters

Kwa mujibu wa tangazo la wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo, kati ya kura zaidi ya 800,000 kutoka zaidi ya vituo 1,600, Rowhani amejizolea zaidi ya nusu, huku mpinzani wake wa karibu, Meya wa Tehran, Mohammad Baqer Qalibaf, akipata kura 126,000.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mohammad Najjar, amesema kuwa kiwango kikubwa cha watu waliojitokeza kupiga kura kimechelewesha kazi ya kuhisabu kura. Wagombea wote sita wanaonekana kuwa wahafidhina, ingawa Rowhani alijaribu kuwavutia wanamageuzi katika kampeni zake.

Wachambuzi wa siasa za Iran wanasema ushindi huu wa awali wa Rowhani, ambao hata hivyo bado haujamuhakikishia kuwa atashinda kwenye kura za jumla, unaonesha kwamba wapiga kura walibadili mawazo yao katika dakika za lala-salama, kwani hadi siku chache kuelekea upigaji kura, wahafidhina ndio walioonekana kuzimiliki siasa za taifa hilo la Kiislamu.

Bado Rowhani hajawa mshindi wa wazi

Hadi sasa Rowhani, ambaye ni mpatanishi wa zamani wa Iran kwenye mazungumzo ya nyuklia, anaripotiwa kuwa na asilimia 46.6 ya zaidi ya kura 861,000, huku Meya wa Tehrani akiwa na asilimia 14.6. Mpatanishi wa sasa kwenye mazungumzo ya nyuklia, Saeed Jalili, ambaye anafahamika kwa misimamo yake mikali, anaonekana kuwa nafasi ya tatu.

Moja ya vikao vya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na mataifa ya Magharibi.
Moja ya vikao vya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na mataifa ya Magharibi.Picha: picture-alliance/dpa

Iran ina zaidi ya wapiga kura milioni 50 na idadi ya waliojitokeza kupiga kura zao siku ya Ijumaa, ilikuwa kubwa sana. Wanamageuzi wengi wa Iran ambao wamshuhudia miaka mingi ya ukandamizaji wanamuona Rowhani kama kiongozi anayeweza kutoa fursa pana zaidi ya demokrasia.

Nani hasa anaiongoza Iran

Hata hivyo, mwenye nguvu za kuamua sera kuu za nchi hasa si ofisi ya rais wa Iran kwa mujibu wa mfumo wa utawala wa nchi hiyo, bali baraza la kidini linaloongozwa na kiongozi mkuu wa kidini, ambaye kwa sasa ni Ayatullah Ali Khamenei. Baraza hilo, pamoja na walinzi wake wa kijeshi, wanabakia kuwa taasisi ya juu kabisa kimaamuzi, likiwemo suala nyeti la nyuklia na uhusiano kati ya Iran na mataifa ya Magharibi.

Mmoja wa wapiga kura ´nchini Iran, baada ya kupiga kura yake siku ya Ijumaa.
Mmoja wa wapiga kura ´nchini Iran, baada ya kupiga kura yake siku ya Ijumaa.Picha: IRNA

Hata Rowhani mwenyewe si mgeni kwenye siasa za ndani za baraza hilo na aliwahi kuliongoza Baraza la Usalama la Taifa na kupewa jukumu zito la kuwa mjumbe wa Iran kwenye mazungumzo ya nyuklia mwaka 2003.

Kwa hivyo, hata akiwa yeye ndiye mrithi wa Rais Mahmoud Ahmedinejad, bado hakutarajiwi mabadiliko ya msingi kuelekea sera za nyuklia na mahusiano ya Iran na mataifa ya nje.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo