Rouhani yuko tayari kulinda maeneo matakatifu
18 Juni 2014Akiyataja maeneo hayo matakatifu ya Karbala, Najaf, Kadhimiyah na Samarra, Rais Rouhani amesema Iran itayalinda maeneo hayo dhidi ya magaidi.
Akizungumza kupitia televisheni ya kitaifa nchini Iran rais huyo amesema, kwa sasa watu wengi nchini humo wamethibitisha kuwa tayari kujitolea kupigana na magaidi na kulinda maeneo matakatifu ambayo yamekuwa yakitembelewa na maelfu ya mahujaji kila mwaka.
Siku ya Jumamosi Rais Rouhani aliahidi kuisasidia serikali ya Waziri Mkuu wa Iraq Nouri al Maliki iwapo itaombwa kufanya hivyo. Hata hivyo kwa sasa hakuna msaada wa aina yoyote ule Iraq ulioiomba kutoka Iran.
Hatua ya kujitolea kwa Iran inafanyika baada ya kiongozi mkuu wa kidini wa madhehebu ya Washia nchini humo Ayatollah Ali al-Sistani, kutoa wito wa watu kujitolea kupigana na kundi la kigaidi la dola la kiislamu la Iraq na eneo la bahari ya Sham, ISIL.
Kundi hilo kwa sasa linadhibiti miji mikubwa ya Iraq ikiwemo Mosul na Tikrit na wanapigana kaskazini mwa Baghdad. Kundi la ISIL linawataja washia kuwa waasi.
Aidha Waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Colin Powell ametoa wito wa kudhibitiwa kwa wanamgambo na mazungumzo ya kidiplomasia kuanza mara moja.
Saudi Arabia yaonya juu ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe Iraq
Wakati huo huo Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Saudi Arabia mwanamfalme Saud al-Faisal, amesema hali ya usalama inayozidi kuwa mbaya nchini Iraq inaweza kuiweka nchi hiyo katika hatari ya kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mwanamfalme Saud al-Faisal aliyasema haya katika mkusanyiko wa viongozi wa kiarabu na wakiislamu mjini Jeddah.
Hatua ya kusogea mbele kwa wanamgambo wa ISIL wanaodaiwa kuwa na mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, iliifadhaisha serikali inayoongozwa na washia ya Nouri al Maliki wiki iliopita ambapo wanajeshi wake wameiacha miji kadhaa kaskazini mwa Iraq.
Kwa sasa afisa mkuu wa usalama wa Iraq amesema wanamgambo hao wa ISIL wameuteka mtambo mkubwa wa mafuta katika eneo la Baiji kilomita 200 kutoka Kaskazini mwa Baghdad.
Huku hayo yakiarifiwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki amesema ubalozi wake mjini Baghdad unafanya uchunguzi juu ya ripoti zinazosema kwamba wanamgambo wamewateka nyara wafanyakazi 60 wa ujenzi wakiwemo raia 15 wa uturuki karibu na mji wa Kirkuk.
Inasemekana wafanyakazi hao waliotekwa ni raia kutoka Pakistan, Bangladesh, Nepal na Turkmenistan. Ripoti hii inasemekana kutolewa na mmoja wa wafanyakazi aliyetekwa na baadae kuachiwa na wanamgambo hao.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu