1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rouhani na Erdogan wasaini mikataba ya biashara

7 Aprili 2015

Rais wa Uturuki Tayyip Recep Erdogan na mwenzake wa Iran Hassan Rouhani wamekubaliana leo kuimarisha biashara na kusaini mikataba kadhaa, lakini walikwepa kuzungumzia tofauti zao kuhusiana na mzozo wa Yemen.

https://p.dw.com/p/1F3ij
Iran Türkei Staatsbesuch Erdogan
Picha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Ziara ya siku moja ya Tayyip Erdogan nchini Iran imekuja wakati uhusiano baina ya serikali ya Uturuki na Iran – ambayo tayari umeharibiwa na migawanyiko kuhusiana na hali ya Syria, umegubikwa na matukio ya nchini Yemen, ambako wanaunga mkono pande zinazopingana.

Erdogan anaishutumu Iran kwa kujaribu kuitawala kanda ya ya Mashariki ya Kati. Baadhi ya wabunge wa Iran walitaka ziara hiyo ifutiliwe mbali, wakati mwanasiasa mmoja akisema rais wa Uturuki alitaka kuujenga upya Utawala wa Ottoman.

Lakini wachambuzi wanasema mzozano baina ya majirani hao wawili utaamuliwa na utegemezi wa kiuchumi – maana Uturuki inahitaji gesi inayotoka Iran wakati nayo Iran inayokabiliwa na vikwazo vya nchi za magharibi ikihitaji kwa kiasi kikubwa masoko ya nje

Iran Türkei Erdogan mit Rohani in Teheran
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan akikaribishwa na mwenyeji wake Hassan Rouhani nchini IranPicha: Tasnim

Viongozi hao wawili wametia saini mikataba minane na wakakabiliwa na wakati mgumu kufafanua na kusisitiza haja ya kuwepo ushirikiano mpana wa kiuchumi, huku Erdogan akisema kuwa nchi hizo mbili zipo nyuma sana ya lengo la kuongeza kiwango cha biashara hadi kufikia dola bilioni 30

Biashara baina ya Iran na Uturuki ilifika kiwango cha jumla cha karibu dola bilioni 14 katika mwaka wa 2014. Waziri huyo mkuu pia amesema Uturuki na Iran zinapaswa kuanza kufanya biashara kwa kutumia sarafu za nchi zao badala ya dola au euro ili kuepukana na udhaifu wa ubadilishanaji fedha za kigeni.

Wakizungumza katika mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari, Erdogan na Rouhani walipuuzilia mbali mvutano wa kikanda, bila kutoa maelezo yoyote ya wazi.

Erdogan alisema haiangalii hali ya mambo nchini Yemen kwa msingi ya madhebu maana haimhusu kama ni Shia wala Sunni. Kinachompa wasiwasi ni Waislamu kwa jumla na hivyo lazima mgogoro huo wa umwagaji damu na vifo lazima ufikishwe kikomo.

Erdogan ambaye ni Muislamu wa madhehebu ya Sunni, anaunga mkono operesheni ya kijeshi inayoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen. Iran inaunga mkono waasi wa Kishia wa kabila la Houthi. Rouhani amesema wote wanaamini kuwa ni muhimu kwao kushuhudia kumalizika kwa vita na umwagaji damu nchini Yemen haraka iwezekanavyo.

Mwandishi: Bruce Amani/reuters
Mhariri:Hamidou Oummilkheir