Ronaldo: Bado sijafikiria kustaafu soka
2 Septemba 2021Nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 ameivunja rekodi ya muda mrefu iliyokuwa inashikiliwa na gwiji wa timu ya taifa ya Iran Ali Daei aliyefunga mabao 109.
Ronaldo, ambaye amejiunga tena na Manchester United akitokea Juventus alifunga mabao mawili katika dakika za mwisho ya mechi ya kufuzu kombe la dunia dhidi ya Ireland, na kuisaidia timu yake kupata ushindi muhimu wa mabao 2-1 jana Jumatano.
Ronaldo, ambaye ni mfungaji bora kwenye ligi ya mabingwa barani Ulaya na pia anaongoza chati ya ufungaji magoli katika historia ya Real Madrid, aliiongoza nchi yake kuibuka mabingwa wa mashindano ya Ulaya Euro mwaka 2016.
"Rekodi zote nilizozivunja katika maisha yangu ya soka, hii ni maalumu kabisa kwangu na ni miongoni mwa mafanikio ya kujivunia," aliandika katika mtandao wake wa Instagram.
Ronaldo amekuwa mchezaji wa kwanza kushiriki katika mashindano matano ya Ulaya, na alishinda kiatu cha dhahabu katika mashindano ya mwaka huu ya Euro 2020.
Anaweza kuifikia rekodi ya kushiriki katika mashindano matano ya kombe la Dunia iwapo timu yake ya taifa itafuzu kushiriki dimba la Qatar mwaka ujao.
Mshindi huyo mara tano wa tuzo ya mchezaji bora duniani Ballon d'Or, amedokeza kuwa hana nia ya kuustafu soka la kimataifa hivi karibuni.
"Asante Ureno. Asante kwa wachezaji wenzangu na hata wapinzani kwa kuniwezesha kufanikisha safari hii isiyosahaulika. Tuendelee kukutana viwanjani kwa miaka mengine ijayo. Bado sijafunga hesabu zangu."
Ureno inacheza na Qatar katika mechi ya kirafiki mnamo siku ya Jumamosi kabla ya kusafiri kwenda kuchuana na Azerbaijan mnamo Septemba 7.