Romney ateuliwa rasmi kuwa mgombea urais kwa niaba ya chama cha Republican
29 Agosti 2012Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 65 anatarajiwa kuukubali rasmi uteuzi huo katika hotuba atakayoitoa hapo kesho ambapo mkutano mkuu wa chama cha Republican unafikia kilele baada ya siku tatu .Akizungumza kwenye mkutano huo mke wa Romney Ann aliwaambia wajumbe kwamba mumewe hatashindwa. Aliwaabia wajumbe kwa moyo wa uthabiti kwamba Romney ndiye mtu atakaeiinua Marekani.
Amesema kila Mmarekani anaefikira juu ya nani anapaswa kuwa Rais ajae ajue kwamba hakuna ataekuwa na bidii kubwa zaidi.Hakuna atakaejali zaidi na hakuna atakaefanya kila kitu kama ,Romney ili kuifanya Marekani pawe mahala bora zaidi pa kuishi
Katika hotuba yake Ann Romney alijaribu kuzigusa nyoyo za wajumbe wa chama cha Republican na za Wamerekani wote kwa jumla alipouzungumzia upande wa mahaba wa historia ya mumewe.Alikumbusha kwamba miaka 47 iliyopita,Romney alicheza naye dansa kwa mara ya kwanza.Amesema ingawa mambo siyo mazuri wakati wote, Romney bado anaendelea kumfurahisha.Na kwa hivyo amewataka WaMarekani wawe na imani na mumewe kwani ni mtu anaeipenda Marekani. Mama huyo amesema Romney atawapeleka Wamarekani pazuri kama jinsi alivyompeleka yeye pazuri.
Romney mwenyewe alipanda jukwaani na kutoa shukurani za moyo kwa wajumbe waliomteua kuwa mgombea wao katika uchaguzi wa urais ambapo atapambana na Rais Barack Obama wa chama cha Democrats.
Katika kura za maoni za nchi nzima Romney amesimama sambamba na Rais Obama kabla ya uchaguzi utakaofanyika mnamo mwezi wa Novemba nchini Marekani. Kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wasiokuwa na ajira nchini Marekani,huenda dau la Romney likaenda joshi.
Hata hivyo kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni na Shirika la "ABC News" na gazeti la "Washington Post," Romney yupo nyuma kuhusu kukubalika. Asilimia 40 ya Wamarekani wanampa Romney nafasi ya kutegemea ushindi ,wakati asilimia 51 wamesema hana matumaini ya kushinda.
Wajumbe kwenye mkutano mkuu wa chama cha Republican pia walimpitisha mbunge Paul Ryan kuwa mgombea mwenzi wa Romney katika nafasi ya Makamu wa Rais. Ryan anazingatiwa kuwa nyota ya chama cha Republican inayoinukia. Wajumbe pia waliupitisha mpango wa chama unaosisitiza uongozi wa Marekani duniani. Kulingana na mpango huo, Marekani, kwa njia ya mafumbo itazitaka nchi za Ulaya zisipunguze bajeti zao za ulinzi. Haki ya kumiliki silaha pia inasisitizwa katika programu iliyopitishwa na wajumbe wa chama cha Republicana kwenye mkutano wao mkuu unaofanyika Tampa Florida.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Euro news/ZA/Afpe
Mhariri: Josephat Charo