ROME:Hatari ya mafua ya ndege Afrika Mashariki.
19 Oktoba 2005Shirika la Chakula Duniani-FAO limesema kuwa kusambaa kwa virusi vinavyosababisha homa kali ya mafua katika eneo la Afrika Mashariki,kunaweza kuongeza uwezekano wa kubadilika na kuwa homa kali ya mafua kwa wanadamu.
Shirika hilo limeonesha matumaini yake kuwa Romania na Uturuki zitafanikiwa kudhibiti haraka kuenea kwa maradhi hayo ya homa ya mafua ya ndege aina ya H5N1,lakini hapo hapo likaonesha mashaka kuwa ndege wanaohama hivi sasa wanaweza kusambaza ugonjwa huo hadi katika eneo la mashariki mwa Afrika.
Hivi sasa nchini Afrika Kusini mamlaka zinazohusika zimeanza kukusanya mabaki ya vinyesi vya ndege walio safarini kupitia pwani yake ya mashariki na kufanya uchunguzi kama vimebeba vijidudu vya homa ya mafua ya ndege.
Baadhi ya wataalam wamesema Afrika Kusini huenda isikabiliwe na kitisho hicho kutokana na ndege hao kupita mbali na pwani yake na kuondoa uwezekano wa kugusana na mifugo aina ya ndege wafugwa nyumbani.Lakini hata hivyo bado hatari ipo.