ROME wanajeshi wa zamani wa Ujerumani wahukumiwa kifungo cha maisha gerezani
23 Juni 2005Matangazo
Mahakama moja ya kijeshi nchini Itali imewahukumu wanajeshi 10 manazi wa Ujerumani, walio na umri zaidi ya miaka 80, kifungo cha maisha gerezani kwa mauaji ya halaiki wakati wa vita vya pili vya dunia. Mahakama hiyo mjini Rome imeamuru wanajeshi hao, ambao kesi yao ilisikilizwa bila wao kuwepo mahakamani, walipe faini na gharama za korti.
Manazi hao wa zamani walishtakiwa kwa kuwaua watu 560 katika kijiji cha mlima wa Tuscan cha Sant Anna di Stazzema karibu na Lucia mwaka wa 1944, siku chache baada ya kukombolewa kwa Florence na wanajeshi wa Uingereza.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, bwana Otto Schily, aliyaeleza mauaji hayo ya halaiki kama aibu kubwa, wakati wa sherehe za kuweka mashada ya maua mapema mwaka huu.