1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ROME-Ulinzi waimarishwa kwa anga la Rome kwa jili ya viongozi wanaohudhuria mazishi ya Baba Mtakatifu.

7 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFPd

Serikali ya Italia imekifunga kiwanja cha ndege cha pili cha mjini Rome kwa matumizi ya ndege za abiria na kuimarisha sheria ya kuzuia ndege yoyote ya abiria kuruka katika anga la mji huo leo,kwa ajili ya usalama wa viongozi zaidi ya 200 kutoka mataifa mbalimbali wanaokusanyika kwa ajili ya mazishi ya Baba Mtakatifu,Yohanna Paulo wa pili.

Katika hatua nyingine isiyowahi kutokea,magari katika mji wa Rome yamezuiwa kutembea kuanzia saa nane usiku kesho Ijumaa siku ya mazishi yenyewe,hadi saa kumi na mbili jioni.

Uwanja wa ndege wa Ciampino utaendelea kufungwa hadi usiku wa manane kesho Ijumaa na halikadhalika kiwanja kikubwa cha ndege cha Fiumicino mjini Rome,pia kimepunguza uwezo wake wa kuhudumia ndege kwa asilimia 30 kutokana na kufungwa kwa anga la mjini huo.

Tayari sheria ya kuzuia ndege za kiraia kuruka katika anga ya Rome ilianza kufanyakazi tangu jana na itaendelea hadi kesho,huku helikopta za polisi zikiwa zinajivinjari katika anga la Vatican,ambapo maelfu ya waombolezaji wanaendela kujipanga kuuaga mwili wa Baba Mtakatifu.

Polisi na wanajeshi wanaofikia 10,000 wanafanya kazi ya ziada kudhibiti umati wa watu katika vitongoji jirani na Vatican,huku kikosi cha mbwa maalum wenye utaalam wa kunusa mabomu wakiwa pia wamekwekwa katika eneo hilo. Watu wanaokwenda kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho hawaruhusiwi kubeba mfuko wa aina yoyote.

Viongozi kutoka nchi 100 wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya Baba Mtakatifu kesho.Baba Mtakatifu Yohanne Paulo wa pili,alifariki dunia siku ya Jumamosi iliyopita baada ya kipindi kirefu cha kuugua.