Rome Uchaguzi wa Pope mpya wakaribishwa na wengi lakini baadhi ya Wakatoliki watia shaka.
20 Aprili 2005Uchaguzi wa kanisa Katoliki wa kadinali Joseph Ratzinger, mwenye msimamo wa kihafidhina zaidi katika masuala ya kidini , kuwa Pope mpya ambaye atajulikana kama Pope Benedict wa kumi na sita, umekubalika kwa kiasi kikubwa duniani kote na wakatoliki wengi lakini pia hatua hiyo imeleta hali shaka shaka. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 78 mzaliwa wa jimbo la Bavaria nchini Ujerumani akiwa pia Pope wa kwanza Mjerumani katika karibu miaka 500, alichaguliwa na makadinali 115 katika Vatican jana Jumanne.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa amesema kuwa Pope Benedict anakuja na uzoefu mkubwa katika ofisi hiyo ya kidini.
Kansela Gerhard Schroeder wa Ujerumani amesema kuwa Ratzinger atakuwa chaguo muhimu badala ya pope wa zamani marehemu pope John Paul wa pili.
Wakati wengi kati ya Wakatoliki bilioni 1.1 duniani wanashangilia kuchaguliwa kwa Ratzinger kama alama ya kuendelea kwa uongozi wa kanisa hilo, kumekuwa na mshangao miongoni mwa watetezi wa haki za wanawake na wasenge na Wakatoliki wenye msimamo wa kati wakitaka mageuzi. Msomi maarufu wa masuala ya dini Hans Kung amesema uchaguzi wa Ratzinger unakatisha tamaa.
Watu wanaotia shaka shaka katika uchaguzi huo pia ni pamoja na Wakatoliki wa America ya kusini na Wanigeria ambao walitaka Pope kutoka katika maeneo yao kama mtetezi wa watu masikini duniani.
Askofu mkuu wa kanisa la Anglikan nchini Afrika kusini Desmond Tutu ameeleza kukatishwa kwake tamaa na uchaguzi wa Joseph Ratzinger jana kuwa Pope mpya, akisema kuwa kiongozi huyo ni mhafidhina asiyetaka kabisa mabadiliko, na ambaye haendi na wakati.