ROME-Serikali ya Italia yapinga ripoti ya jeshi la Marekani juu ya mauaji ya ofisa wake wa usalama nchini Iraq.
27 Aprili 2005Serikali ya Italia na vyama vya upinzani nchini humo,vimeshutumu ripoti iliyotolewa na jeshi la Marekani kufuatia mauaji ya afisa wa usalama wa nchi hiyo,ambaye alishiriki katika kuachiwa huru kwa mwandishi wa Kitaliano,Giuliana Sgrena aliyeshikiliwa mateka nchini Iraq.
Machunguzi wa Kimarekani wametoa ripoti yao ikionesha kuwa wanajeshi wa Marekani hawakufanya makosa wakati mauaji ya afisa usalama huyo Nicola Calipari yalipotokea mwezi uliopita wa Machi.
Wanajeshi wa Marekani walilifyatulia risasi gari lililokuwa na mwandishi huyo wa habari,ambapo Calapiri alikuwa akimsindikiza kuelekea uwanja wa ndege wa Baghdad,baada ya kufanikisha kuachiwa huru kwa mwandishi huyo aliyekuwa ametekwa na waasi nchini Iraq.
Mwandishi huyo Bibi Sgrena pia ametoa shutuma zake kutokana na ripoti hiyo ya jeshi la Marekani na kusema kuwa afisa wa usalama aliyekuwa anamsindikiza aliuliwa kwa makusudi.