ROME : Prodi yumkini kuongoza tena serikali
24 Februari 2007Rais wa Italia leo hii ataamuwa iwapo Romano Prodi anastahiki kupewa nafasi nyengine ya kuongoza nchi kama waziri mkuu baada ya uasi kwenye bunge kulazimisha kujiuzulu kulikofadhaisha taifa.
Washirika wa Prodi wanasisitiza kwamba wamerekebisha tafauti zao katika serikali yake ya mseto ya mrengo wa shoto wa wastani ambayo kusambaratika kwake kwa ajabu wakati wa kupigwa kura bungeni katika masuala ya sera ya kigeni hapo Jumaatano kumezusha uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi wa haraka baada ya kuwa madarakani kwa miezi tisa tu.
Rais Giorgio Napolitano hatazamiwi kuitisha tena uchaguzi licha ya kuiacha nchi hiyo katika hali ya kuaguwa hapo jana iwapo atamrudisha Prodi au atamchaguwa kiongozi mwengine kuunda serikali ya mpya ya mseto. Prodi ameishawishi serikali yake ya mseto kukubaliana na mpango wa kisiasa wa vipengele 12 unaojumuisha uungaji mkono uwekaji wa wanajeshi 2,000 wa Italia nchini Afghanistan.
Mahasimu wa Prodi akiwemo waziri mkuu wa zamani wa Italia Silvio Berlusconi wanataraji Rasi Napolitano atamfungisha virago Prodi.