1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rome. Pope mpya wa kanisa Katoliki aendesha misa , Vatican.

20 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFLA

Kiongozi mpya wa kanisa katoliki Pope Benedict wa kumi na sita ameendesha misa leo kwa mara ya kwanza katika Vatican. Uchaguzi wa kiongozi huyo mzaliwa wa jimbo la Bavaria nchini Ujerumani Joseph Ratzinger mwenye msimamo wa kihafidhina zaidi katika masuala ya kidini, umekubalika kwa kiasi kikubwa duniani kote na wakatoliki wengi lakini pia hatua hiyo imeleta hali ya shaka shaka kwa baadhi ya watu.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa amesema kuwa Pope Benedict wa kumi na sita anakuja na uzoefu mkubwa katika ofisi hiyo ya kidini.

Kansela wa Ujerumani Gerhard Schroeder amesema kuwa Ratzinger atakuwa chaguo muhimu badala ya pope wa zamani marehemu pope John Paul wa pili.

Wakati wengi kati ya Wakatoliki bilioni 1.1 duniani wanashangilia kuchaguliwa kwa Ratzinger kama alama ya kuendelea kwa uongozi wa kanisa hilo, kumekuwa na mshangao miongoni mwa watetezi wa haki za wanawake na wasenge na Wakatoliki wenye msimamo wa kati wakitaka mageuzi.

Msomi maarufu wa masuala ya kidini Hans Kung amesema uchaguzi wa Ratzinger unakatisha tamaa.

Watu wanaotia shaka shaka katika uchaguzi huo pia ni pamoja na wakatoliki wa Amerika ya kusini na Wanigeria ambao walitaka pope kutoka katika maeneo yao , kama mtetezi wa watu masikini duniani