ROME-Maelfu ya waombolezaji wanazidi kumiminika kuuaga mwili wa Baba Mtakatifu.
7 Aprili 2005Maelfu ya waombolezaji bado wanazidi kumiminika kwa utulivu,kuuaga mwili wa Baba Mtakatifu Yohanna Paulo wa pili,lakini hata hivyo umati huo unaanza kupungua baada ya kuwepo umati mkubwa zaidi,kiasi cha kuleta hofu siku chache zilizopita.
Wakati huo huo serikali ya Italia,imezidi kuimarisha utaratibu wa kuzuia ndege za abiria kuruka katika anga la mji wa Rome na Vatican.Pia uwanja wa ndege wa pili wa mjini Rome,nao umefungwa kwa ajili ya kuwalinda viongozi 200,kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni,wanaohudhuria mazishi ya Baba Mtakatifu.
Katika shughuli ya kesho ya maziko,walenga shabaha hodari 1,000 wa vikosi vya usalama vya Italia,wanatazamiwa kuchukua nafasi zao katika maeneo muhimu kuzunguka viwanja vya Mtakatifu Petro.Kwa ujumla kuna walinda usalama 10,000 wamewekwa kukabiliana na lolote na kuwalinda viongozi katika maziko,pamoja na mamilioni ya watu waliowasili Rome tangu siku chache zilizopita.