1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ROME : Maelfu waadhimisha siku ya wafanyakazi

1 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFHZ

Maelfu ya wafanyakazi leo hii wameandamana katika miji mikuu ya dunia kuanzia Moscow,Paris hadi Manila kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani May Day kwa madai ya mazingira bora ya kazi wakati Baba Mtakatifu mpya wa Kanisa Katoliki akitowa wito wa kuheshimiwa kwa haki za wafanyakazi.

Papa Benedikt wa 16 akiwahutubia zaidi ya mahujaji 50,000 katika uwanja wa St.Peter amesema anataraji wataendelea na udugu wao wa Kikristo kwa sababu mshikamano,haki na amani ni nguzo ambayo kwayo imejenga familia ya binaadamu.

Papa huyo mpya ambaye wiki iliopita alisema atatumia uongozi wake kuleta umoja wa Wakristo pia ametuma salamu hususan kwa Makanisa ya Kiorthodox ambayo leo yanaadhimisha Pasaka.

Leo ikiwa ni siku muhimu kabisa katika kalenda ya Kanisa la Orthodox nchini Russia wafanyakazi 20,000 waliandamana mjini Moscow kudai kuongezwa kwa mishahara ili iowane na gharama za hali ya maisha.

Mjini Paris maandamano ya wafanykazi yametiwa kiwingu na kugawika ndani ya vyama vya wafanyakazi juu ya katiba iliopendekezwa ya Umoja wa Ulaya ambayo itapigiwa kura ya maoni nchini Ufaransa hapo tarehe 29 mwezi wa Mei.

Mjini Berlin polisi ya Ujerumani imewatia mbaroni watu 65 wakati wa mapambano na waandamanaji wa sera za mrengo wa shoto wakati wa kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani Mei Mosi.Polisi inasema maafisa watatu wa polisi wamejeruhiwa kidogo hata hivyo vurugu hizo zimekuwa sio kubwa kulinganishwa na zile za mwaka jana ambapo polisi 200 walijeruhiwa na watu zaidi ya 200 walitiwa ndani.Maandamano ya Mei Mosi limekuwa tukio la kawaida katika mji mkuu huo wa Ujerumani.

Wakati kukiwa na uvumi mwengine wa njama ya mapinduzi dhidi ya Rais Gloria Arroyo wa Ufilipino waandamanaji 3,000 waliandamana kwenye Kasri la Rais mjini Manila huku maelfu ya polisi na wanajeshi wakiwa katika hali ya tahadahari baada ya serikali kulishutumu kundi la magenerali wastaafu kujaribu kuandikisha wanajeshi kufanya mapinduzi.