ROME: Buriani baba mtakatifu lakini nani atakayekurithi?
4 Aprili 2005Baada ya kifo cha baba mtakatifu Yohana Paulo wa pili,makadinali wakikatoliki wanakutana kwa mara ya kwanza hii leo tangu kifo hicho kupanga mazishi yanayotarajiwa kuhudhuriwa na umma mkubwa wa watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Katika kikao hicho cha leo ,makadinali watakula kiapo cha kuweka siri kuhusu utaratibu wote wa kumchagua atakayerithi wadhifa huo.
Mwili wa baba mtakafu utahamishwa kutoka kasri lake huko Vatican hadi katika kanisa la mtakatifu Peter hii leo kwa ajili ya watu kumuaga na kutoa heshima zao za mwisho.
Kifo cha baba mtakatifu kinaombolezwa kote duniani na watu wa dini mbali mbali.
Rais wa Ujerumani Horst Kohler katika risala yake amemtaja papa kuwa mtumishi wa kweli wa kanisa lake.
Viongozi mbali mbali wa kisiasa hapa Ujerumani ikiwa ni pamoja na Kansela Gerhard Schroder wametoa risala zao kwa kifo cha baba mtakatifu.
Mazishi ya kiongozi huyo mwenye miaka 84 yanatarajiwa kufanyika kati ya siku ya Alhamis au ijumaa ijayo.