ROME: Baba Mtakatifu atazamiwa kuhubiri hadharani
17 Septemba 2006Matangazo
Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 anajitokeza hadharani hii leo kwa mara ya kwanza tangu matamshi yake ya kumnukuu mfalme wa karne ya 14 kusababisha hamaki miongoni mwa Waislamu sehemu mbali mbali za dunia.Papa atakapotoka kwenye nyumba yake ya mapumziko Castel Gandolfo karibu na mji wa Rome,kuhubiri kama kawaida yake ya kila Jumapili,huenda akaitumia nafasi hiyo kuzungumza binafsi kuhusu matamshi yaliyosababisha hamaki.Papa tayari amesema anasikitika kuwa hotuba aliyoitoa Jumanne iliyopita imewakasirisha Waislamu.Katika taarifa ya Vatikan iliyotolewa siku ya Jumamosi,Papa amesema anasikitika kuwa sehemu ya hotuba yake imetafsiriwa visivyo.Lakini makundi mengi ya kiislamu yanamtaka Papa binafsi aombe radhi.