ROMA: Watuhumiwa 15 wakamatwa
13 Februari 2007Polisi nchini Italia wamewatia mbaroni watu 15 katika uvamizi dhidi ya kundi la kigaidi la mrengo wa kushoto uliofanywa nchini kote. Kundi hilo lina uhusiano na kundi la Red Brigades lililoihangaisha Italia katika miaka ya 1970 na 1980. Watu hao wamekamatwa katika miji ya Milan, Turin, Padua na miji mingine ya kaskazini mwa Italia.
Katika taarifa yake polisi nchini Italia wamesema washukiwa waliokamatwa wanashtakiwa kwa kuwa na mafungamano angamizi na kwa kuunda kundi lenye silaha.
Waziri wa mambo ya ndani wa Italia, Giuliano Amato, amesema huenda serikali imefaulu kuzuia shambulio lakini hakutoa maelezo zaidi. Kundi la Red Brigades lilifanya mashambulio mabaya ikiwa ni pamoja na utekaji nyara na mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Italia, Aldo Moro, manmo mwaka wa 1978.