ROMA: Siasa uwanja wa fujo, Berlusconi nae ajiuzulu.
21 Aprili 2005Waziri mkuu wa Italy Silvio Berlusconi tayari amewasilisha stakabadhi za kujiuzulu kwa rais Carlo Azeglio Ciampi ambae amemtaka aendelee kubaki kama msimamizi katika mazungumzo na wahusika wa chama cha mseto yenye lengo la kuunda serikali mpya.
Berlusconi aliwaeleza waandishi wa habaari mjini Roma kuwa anataraji kuyakamilisha mazungumzo hayo kufikia mwisho wa wiki ijayo.
Na iwapo mazungumzo hayo yatashindwa kuafikiana juu ya kuundwa kwa serikali mpya ya Italy basi rais Carlo Azeglio Ciampi atawajibika kulivunja bunge la nchi hiyo na kuamuru uchaguzi wa mapema.
Uongozi wa Berlusconi uliingia utata baada ya chama kimoja katika mseto uliounda serikali hapo awali kujiondoa siku ya ijumaa na huenda chama kingine pia kikajiondoa katika mseto huo kufuatia matokeo mabaya katika uchaguzi uliomalizika hivi punde.