Robo ya watoto chini ya miaka 5 wana uhaba mkubwa wa chakula
6 Juni 2024Taarifa hiyo inamaanisha kuwa, zaidi ya watoto milioni 180 kote duniani wako hatarini kupata athari zinazotokana na ukosefu wa chakula katika ukuaji wao.
Kulingana na ripoti hiyo mpya ya Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF iliyochapishwa Jumatano, upungufu mkubwa wa chakula kwa watoto, unawagusa watoto wanaoishi kwa kupata milo dhaifu kupindukia na kuwa wanaishi kwa kutegemea makundi mawili pekee ya vyakula.
Soma zaidi: Watoto 68,000 Nepal wahitaji msaada
Akifafanua zaidi juu ya utafiti huo, mwandishi mkuu wa ripoti hiyo Harriet Torlesse, amesema kuwa watoto 440 million wenye chini ya miaka mitano wanaoishi katika mataifa 100 yenye uchumi wa kati hawapati mlo kamili kila siku. Naye Mkuu wa shirika hilo la kuhudumia watoto Catherine Russell ameeleza kuwa watoto Milioni 181 kati ya milioni 440 waliotajwa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula hali inayosababisha wapate utapiamlo.
Mataifa 20 yameathiriwa zaidi na upungufu wa chakula kwa watoto
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, umasikini wa upatikanaji wa chakula uliokithiri kwa watoto umejitokeza zaidi katika mataifa 20 yenye hali mbaya yakiwemo Somalia ambamo asilimia 63, wameathiriwa. Mataifa mengine ni Guinea yenye asilimia 54 percent, Guinea-Bissau ikiwa imeathirika kwa asilimia 53 na athari ya hali hiyo kwa watoto huko Afghanistan ni asilimia 49.
Ripoti hiyo imebainisha pia kuwa, katika Ukanda wa Gaza ambako jeshi la Israel linafanya mashambulizi baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7, hali ya chakula na mfumo wa afya ni mbaya.
Soma zaidi:Tatizo la Utapiamlo latishia kizazi kijacho cha Afghanistan
Tangu mwezi Desemba mwaka jana hadi Aprili mwaka huu shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa limefanya awamu tano za ukusanyaji taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu kutoka katika familia zinazopokea misaada kwenye eneo hilo. Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa watoto tisa kati ya 10 wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.
Lilibaini pia maendeleo madogo katika kushughulikia mzozo huo kwa muongo mmoja uliopita na hivyo limetoa wito wa kutatuliwa kwa mzozo huo, kuboreshwa kwa huduma za jamii na misaada ya kiutu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupita kiasi.
UNICEF limeomba pia mfumo wa usindikaji wa chakula uboreshwe kote duniani, kwa kuwa vinywaji vyenye sukari nyingi na vyakula vilivyosindikwa kupitiliza vimekuwa vikitafutiwa masoko kwa fujo kwa wazazi. Limesema sasa imekuwa ni kawaida mpya kwa familia kuwalisha watoto vyakula hivyo.