Robo ya raia wanaouawa Yemen ni watoto
23 Machi 2021Ripoti ya shirika hilo iliyotolewa Jumanne (Machi 23) ilisema kuwa zaidi ya watoto 2,300 waliuawa baina ya mwaka 2018 na 2020, ingawa ilisisitiza kuwa idadi kamili inaweza kuwa kubwa zaidi ya hiyo.
Mkurugenzi wa shirika hilo nchini Yemen, Xavier Joubert, alisema kwamba watoto wamekuwa wakipitia kipindi kigumu kabisa kwa kipindi cha miaka sita sasa, ambapo takribani kila siku wanauwa na kujeruhiwa.
Ripoti hiyo ilitoka siku chache baada ya Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kusema kwamba watoto wanane waliuawa na 33 kujeruhiwa mwezi huu pekee.
Mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen, Phillippe Duamelle, alisema mauaji hayo yalifanyika kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo majimbo ya Taiz na Hodeida, ambako mapigano kati ya vikosi vya serikali inayotambuliwa kimaitaifa na vile vya waasi wa Kihouthi wamezidisha mapigano katika siku za hivi karibuni.
Saudi Arabia yataka kusitishwa mapigano
Siku ya Jumatatu (Machi 22), Saudi Arabia ilitangaza mpango wa kusitisha mapigano na kuwataka waasi hao kuukubali. Mpango huo unajumuisha kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Sanaa, ambao umezingirwa kwa mwaka wa sita sasa.
Hata hivyo, Wahouthi waliukataa mpango huo wakisema hauna jambo jipya.
"Pande zote za mzozo huu lazima zitekeleze makubaliano ya kusitisha mapigano haraka iwezekanavyo. Usitishaji huo wa mapigano lazima utumike kujenga amani ya kweli na suluhisho la kisiasa, kwani ndiyo njia pekee ya kukomesha janga hili la kibinaadamu." Alisema Joubert.
Misaada ya kibinaadamu yapunguwa
Kama yalivyo mashirika mengine ya misaada ya kibinaadamu, Save the Children lenye makao yake makuu London nchini Uingereza limekabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha za ufadhili, ambapo mwaka huu lina upungufu wa asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka jana, hali inayoashiria kuyaweka kwenye hatari kubwa zaidi maisha ya watoto wanaotegemea misaada.
Mkuu wa shirika hilo, Janti Soeripto, alisema kwamba kuna uwezekano ukame mkubwa unaokhofiwa kutokea hivi karibuni, huenda ukawauwa maelfu ya watoto wa Yemen.
Taifa hilo la Arabuni limekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2014, pale Wahouthi walipochukuwa udhibiti wa mji mkuu, Sanaa, na sehemu kubwa ya eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, na kuilazimisha serikali ya Rais Abed Rabbo Mansour Hadi kukimbilia kusini, na kisha Saudi Arabia.
Saudi Arabia ikiungwa mkono na Marekani iliunda muungano wa kijeshi na kuivamia Yemen mwaka 2015 kujaribu kumrejesha Hadi madarakani, lakini watu 130,000 wameshauwa na bado hakujapatikana suluhisho lolote.