1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuvaana na Sweden katika robo fainali

20 Juni 2015

Michuano ya robo fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake inaanza leo nchini Canada, wakati Ujerumani itashuka dimbani na Sweden mjini Ottawa.

https://p.dw.com/p/1Fk4d
Frauenfussball-WM 2015 Kanada
Picha: picture-alliance/dpa

Sweden ambayo imekuwa na kazi ngumu kufikia duru hii inaelekea bado ina kibarua kizito. Timu hiyo ya wanawake ambayo iko nafasi ya tano katika orodha ya kimataifa, itaumana leo na Ujerumani inayoshika nafasi ya kwanza duniani katika soka la wanawake.

Ujerumani ambayo sawa na Marekani zimeshanyakua kombe hilo mara mbili kila moja tangu mashindano hayo ya timu za wanawake yaanze 1991, ilimaliza nafasi ya kwanza katika kundi lake ambapo ilifunguwa dimba kwa kuipa funzo Cote d´Ivoire la mabao 10-0 kabla ya kutoka sare na Norway 1-1 na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Thailand.

Marekani itakuwa mjini Edmonton kupambana na Colombia, iliowashangaza wengi ilipoibwaga Ufaransa 2-0 katika duru ya awali. Ufaransa kwa upande wake itacheza na Korea Kusini Jumapili mjini Montreal wakati hiyo hiyo kesho Brazil itatoana jasho na Australia katika uwanja wa Moncton na Cameroon mwakilishi pekee wa Afrika aliyesalia katika kombe hilo la dunia baada ya nigeria na Cote d´ivoire kuyaaga itakuwa uwanjani dhidi ya China.

Cameroon ilioko nafasi ya 53 katika orodha ya dunia ni timu ya pili ya Afrika kufanikiwa kuingia duru ya pili ya mtoano katika kombe la dunia la wanawake baada ya Nigeria 1999. Mshindi wa mechi hiyo ataingia robo fainali kuchuana na mshindi wa mechi kati ya Marekani na Columbia.

Wenyeji wa mashindano Canada wanasubiri kuvaana na Uswisi mjini Edmonton hapo kesho. Uingereza itakuwa uwanjani Jumatatu dhidi ya Norway, mabingwa wa kombe hilo 1995. Mabingwa watetezi Japan watacheza na Uholanzi . Fainali ya kombe la kandanda la dunia la wanawake itachezwa Vancouver Julai 5.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Abdu Mtullya