Roberta Metsola spika mpya wa Bunge la Ulaya, ni nani?
18 Januari 2022Roberta Metsola, mwenye umri wa miaka 43 siku zote ameweka wazi kwamba kwake Umoja wa Ulaya sio taasisi ngumu ya urasimu, bali shauku ya kweli.
Sio umoja huo ambao unakumbwa na mzozo, lakini ni sehemu ya kukuza maadili ya Ulaya kwa mradi ambao unaibuka kutoka kwenye majivu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Sasa, mwasasiasa wa kihafidhina kutoka Malta lazima athibitishe kwamba anaweza kuyabadili maneno yake na kuwa vitendo. Siku ya Jumanne Roberta Metsola alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Ulaya mjini Strasbourg, Ufaransa, ambayo pia ni siku aliyotimiza miaka 43 tangu kuzaliwa kwake.
Kuchaguliwa kwa Metsola kunaweza kupongezwa na wengi kama zawadi ya siku ya kuzaliwa kwa mbunge huyo wa Malta, lakini halikuwa jambo la kushangaza.
Katika makubaliano ya pamoja, makundi matatu makubwa ndani ya Bunge la Ulaya, ambayo ni muungano wa vyama vya kihafidhina EPP, muungano wa vyama vya kisoshalisti na wanademokrasia, na muungano wa vyama vya Kiliberali waliamua mwakilishi wa kihafidhina atachukua wadhifa huo katikati ya muhula.
Metsola ambaye chama chake cha Partir Nazzjonalist ni sehemu ya muungano wa EPP ambapo anaonekana kuwa chaguo la wazi kwa vile anaheshimika ndani ya chama hicho na anajulikana kwa kuondoa mivutano.
David Casa, aliyeko kwenye chama kimoja na Metsola na mbunge mwenzake wa Bunge la Ulaya ameiambia DW kwa muhtasari: "wote wamezoea migawanyiko na mizozo. Na kupanda kwa Roberta na umaarufu wake kunathibitisha kwamba bado inawezekana kufanya siasa kwa makubaliano."
Mwanasiasa huyo wa Malta ni mwanamke wa tatu kuwa spika wa Bunge la Ulaya, akifuata nyayo za watangulizi wake kutoka Ufaransa, Simone Veil na Nicole Fontaine.
Bunge la Ulaya ni chombo cha kutunga sheria cha Umoja wa Ulaya ambacho kinawawakilisha wananchi milioni 450 wa umoja huo na huchaguliwa moja kwa moja na wapiga kura wa Umoja wa Ulaya kila baada ya miaka mitano.
Metsola alishindwa kuchaguliwa mara mbili
Video mbili za kampeni zilizoonyeshwa na muungano wa EPP katika mtandao wa kijamii kabla ya uchaguzi, zinaelezea jinsi Metsola anataka kutambuliwa. Mtu aliyetiwa moyo na wanawake wengine wenye nguvu, anataka kuwahamasisha wengine.
Mama huyo mwenye watoto wanne wa kiume anajaribu kuyagawa majukumu ya kifamilia na kazi yake. Mpambanaji ambaye hakati tamaa, pale anapoamini katika jambo fulani.
Metsola alifanikiwa kuchaguliwa kuingia kwenye Bunge la Ulaya mwaka 2013 baada ya kushindwa mara mbili. Tangu wakati huo amekuwa akipanda kwa haraka.
Mwaka 2020 alikuwa mmoja wa makamu wa kwanza wa spika wa Bunge la Ulaya. Kama mjumbe wa Kamati ya Uhuru wa Kiraia, Haki na Masuala ya Ndani, ametetea haki ya kupata hifadhi ndani ya Umoja wa Ulaya.
Wabunge wengi walimpigia debe kwa sababu ya sifa nyingine ambayo mbunge mwenzake wa muungano wa EPP, Stelios Kympouropoulos kutoka Ugiriki aliielezea kama "ujasiri wa kutosha kuwa uso wa bunge shupavu na lenye nguvu."
Wakosoaji waupinga msimamo wa Metsola wa utoaji mimba
Ingawa Roberta Metsola alikuwa mgombea sahihi wa wengi, wengine hasa wabunge wa vyama vya Kijani na vinavyofuata siasa za mrengo wa Kushoto hawana furaha haswa yeye kuwa kiongozi kwa sasa. Hii yote ni kwa sababu mwanasiasa huyo wa Malta siku zote amekuwa akipinga maazimio ndani ya Bunge la Ulaya yanayozitaka nchi za Umoja wa Ulaya kuhalilisha utoaji mimba.
Kwa upande wake Manon Aubry, mwanasiasa wa Ufaransa kutoka chama cha mrengo wa Kushoto ndani ya Bunge la Ulaya, ameiambia DW kwamba anaona hiyo ni ishara mbaya kwa haki za wanawake kote Ulaya. Anawatolea mfano wanawake wa Poland ambao wamekuwa wakipigania haki ya kuwa na maamuzi ya miili yao kwa takribani miaka miwili.
Hata hivyo, Aubry pia anamtambua Metsola kuwa sehemu ya maendeleo ya muungano wa EPP, kwa mfano amekuwa akitetea haki za watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.
Kiongozi wa watu wote wa Ulaya
Casa anasema haoni kama suala la utoaji mimba kuwa ni tatizo wakati wa kipindi chake cha urais. Anasema ni wazi kwamba Metsola alipaswa kuheshimu maadili yaliyooneshwa mara kwa mara na watu wa Malta. Alikuwa akimaanisha utafiti wa maoni ya umma yanayopinga utoaji mimba katika kisiwa hicho cha Kikatoliki.
Ingawa Manon Aubry mbunge kutoka Ufaransa angependelea kuwa na kiongozi mwingine wa Bunge la Ulaya, anasema muungano wake utakuwa unatafuta mazungumzo na Metsola.
Ameiambia DW kwamba ana matumaini Metsola hatowakilisha tu maslahi ya Malta, bali yale ya Bunge lote la Ulaya. Wabunge wengi huko mjini Strasbourg, mara kwa mara wamekuwa wakilaani matukio ya kupinga utoaji mimba barani Ulaya.
(DW)